Customer Feedback Centre

Ministry of Health

HOSPITALI YA HALMASHAURI, HANDENI MSAADA MKUBWA KWA WATUMIAJI WA BARABARA YA CHALINZE –TANGA

Posted on: September 30th, 2023

Na. WAF, Handeni -Tanga

Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni itakwenda kuwa msaada mkubwa wa kuhudumia majeruhi na kuokoa maisha ya wananchi watakao pata ajali katika barabara ya Chalinze Kwenda Tanga.


Hayo yamebainisha na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Kassim Majaliwa katika hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga ambapo amesema kila mwaka barabara hiyo hutengeneza ajali 1460 .


Aidha amesema kuwa Katika kusogeza Huduma za Afya kwa wananchi Serikali ya awamu ya Sita chini ya uongozi Imara wa Rais Samia Suluhu Hassan imeweka mikakati kujenga zahanati katika kila kijiji, vituo vya afya ambavyo vimeweka mkakati na vijitosheleze kwa Huduma ili kupunguza msongamano katika hospitali za wilaya nchini.


“Lakini pia Rais Samia ameelekeza kila halmashauri kuwa na Hospitali yake ili kusogeza Huduma kwa wananchi na kupunguza msongamano katika Hospitali za Rufaa za Mikoa na Kanda nchini”, ameeleza Mhe. Majaliwa


Mhe Waziri, pia amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa vibali vya kuajili madaktari ambao wamesambazwa katika halmashauri nchini ili kuhakikisha wanatoa Huduma bora za afya kwa wananchi.



Aidha katika ,suala la watumishi Rais Samia anaratibu vizuri kwa kutoa vibali vya ajira wakati wote kulingana na mahitaji husika kwa wakati huo.


Mhe. Majaliwa amesema kuwa mahitaji ya Watumishi wa afya katika hospitali hiyo ni 247 na waliopo sasa ni 47 lakini pia serikali itatoa ajira kwa  watumishi wa sekta ya afya wengine 500.


Amesema kuwa serikali imeshanunua magari ya kubeba wagonjwa na kila halmashauri itapata magari mawili na gari moja kwa ajili ya mkuu wa Kituo kufanya ufuatiliaji wa utoaji Huduma katika vituo vilivyopo kwenye eneo lake.


Rais Samia amefungua wigo kwa mataifa ya nje kuwekeza Tanzania na leo Serikali ya Kuwait imewekeza katika Hospitali ya halmashauri ya wilaya ya Handeni na bado imehaidi kutoa Bilioni 3 ili kuhakikisha ujenzi wa hospitali hiyo unakamilika na kuendelea kutoa Huduma.


“ Nilichokuja kufanya leo ni kuweka jiwe la msingi ujenzi uendelee na nimeaambiwa baadhi ya Huduma zimeaanza kutolewa hapa hivyo kazi iendelee”, ameongeza Mhe. Majaliwa


Katika hatua nyingine, akatoa wito kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kuwashika vizuri hawa wadau kutoka Kuwait ili kuendelea kuwekeza katika miradi mbalimabali ndani ya Halmashauri yao.


Hata hivyo ametoa maelekezo kwa Meneja wa TARURA wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kutengeneza barabara ya kufika katika hospitali hiyo ili kuepuka adha ya kufika katika hospitali hiyo kipindi cha mvua.