Customer Feedback Centre

Ministry of Health

HOSPITALI YA BENJAMINI MKAPA YAMUAGA MTOTO WA 14 KUPONA SELIMUNDU

Posted on: September 5th, 2024

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imemuaga Faith Mwinula (9), ambaye ni mtoto wa kumi na nne kupona ugonjwa wa selimundu baada ya kupandikizwa uloto.


Ugonjwa wa Selimundu ni ugonjwa wa kuzaliwa nao kutokana na kuurithi kutoka kwa wazazi wa mtoto kupitia vinasaba.


Akiongea na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma cha Hospitali, Mama mzazi wa mtoto, Pendo Luteja, amesema alipata taarifa kuwa BMH wanatoa huduma hiyo kupitia chombo Cha habari Cha televisheni (TV).


"Niliona kwenye TV wakati Mhe. Ummy (Waziri wa zamani wa Afya) anamtambulisha mtoto wa kwanza kupona sikoseli Bungeni baada ya kupata matibabu katika Hospitali ya Benjamin Mkapa," amesema mama mzazi wa Faith, ambaye ni mkazi wa Musoma, mkoani Mara.


Pendo amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali, madaktari na wauguzi kwa kuanzisha huduma hiyo, kwani imesaidia kuokoa uhai wa binti yake.


"Namshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali kwa kufikiri na hatimaye kuanzisha huduma. Kwa kweli, imesaidia kuokoa uhai wa mwanangu," ameongeza.


Kwa upande wake, Daktari William Lloyd, wa kitengo Cha upandikizaji uloto ameshukuru wazazi wa Faith kwa kuiamini BMH.


"Tunawashukuru wazazi wa Faith kwa kutuamini na kumleta binti yao kupata matibabu ya sikoseli hapa," amesema Dkt Lloyd, ambaye pia ni Mratibu wa Huduma ya Upandikizaji Uloto wa BMH.


Faith ni mgonjwa wa kwanza kupandikizwa uloto kutoka kwa mchangiaji ambaye kundi la damu ni tofauti.