Customer Feedback Centre

Ministry of Health

"HEALTH BASKET FUND" YAZIDI KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA NGAZI YA MSINGI

Posted on: May 16th, 2025

Na WAF, Arusha


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema mafanikio makubwa yamepatikana kupitia Mfuko wa Pamoja wa Afya, ujulikanao kama Health Basket Fund, katika kuimarisha huduma za afya ngazi ya msingi kote nchini. 


Mafanikio hayo kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na uwekezaji wa Serikali ya Denmark chini ya DANIDA INVESTMENT FUND kupitia Benki ya CRDB. 


Kauli hiyo imetolewa na Mfamasia Mkuu wa Serikali, Bw. Daudi Msasi, Mei 16, 2025  wakati akiwasilisha mada kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, katika Mkutano Mkuu wa 30 wa Benki ya CRDB unaofanyika jijini Arusha.


Akizungumza mbele ya wanahisa wa benki, wadau wa sekta ya afya, mashirika ya maendeleo na taasisi za kifedha, Bw. Msasi amesema kuwa, Health Basket Fund imeendelea kuwa nguzo muhimu katika utekelezaji wa Mpango wa Sekta ya Afya wa Miaka Mitano.


Kupitia mfuko huo, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imefanikiwa kuongeza upatikanaji wa dawa, kuimarisha miundombinu ya vituo vya kutolea huduma za afya, pamoja na kuboresha usimamizi wa huduma katika maeneo ya mijini na vijijini.


"Health Basket Fund inachangiwa na nchi rafiki zikiwemo Canada, Switzerland, Denmark (DANIDA INVESTMENT), Ireland na Uingereza. Mashirika ya kimataifa yanayochangia ni pamoja na Benki ya Dunia, UNICEF, UNFPA na KOICA" amesema Bw. Msasi na kuongeza


"Serikali, kwa kushirikiana na wadau hao, hupanga matumizi ya fedha kwa pamoja, husimamia utekelezaji wa miradi, na hufanya tathmini ya afua zote za afya kulingana na mkakati wa sekta ya afya wa miaka mitano," ameongeza Msasi.


Aidha, amesema kuwa vipaumbele vya mfuko huo ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya vituo vya kutolea huduma za afya, kuhakikisha upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba, kuboresha uendeshaji wa vituo, pamoja na kusimamia utekelezaji wa sera, miongozo, sheria na kanuni katika ngazi ya Wizara. Pia, mfumo wa ufuatiliaji na tathmini unaoendelea kuimarishwa katika ngazi ya Wizara, TAMISEMI na halmashauri.


Bw. Msasi asema, Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi kuhakikisha fedha zinazotolewa zinatumika kwa uwazi, kwa kuzingatia vipaumbele vya wananchi na kwa lengo la kupata matokeo chanya katika sekta ya afya.


“Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya bila kikwazo cha kifedha au umbali wa kufikia huduma,” alisisitiza Msasi.


Mkutano huo wa siku mbili umewaleta pamoja washiriki kutoka sekta mbalimbali na kutoa jukwaa la kujadiliana, kubadilishana uzoefu, na kujenga mikakati thabiti ya kuboresha zaidi matumizi ya rasilimali kwa maendeleo endelevu ya sekta ya afya nchini.


Aidha, kwa upande Balozi wa Denmark nchini Mhe. Jesper Kammersgaard ameipongeza  Serikali ya Tanzania kwa  kuendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha Afya za Watanzania zinaendelea kuwa imara kwa mipango madhubuti.