Customer Feedback Centre

Ministry of Health

HAKIKISHENI MNAWEKA MAZINGIRA RAFIKI YA KUZUNGUMZA NA VIJANA KUHUSU VVU NA UKIMWI.

Posted on: November 6th, 2023

Na WAF - Ifakara, Morogoro 

Walimu, wazazi na watoa huduma za Afya ngazi zote wametakiwa kuhakikisha wanaweka mazingira rafiki ya kuzungumza na vijana wa umri kati ya miaka 15-24 juu ya umuhimu wa kushinda vishawishi ili kuwa bora kuweza kufikia ndoto zao.


 Wito huo umetolewa na Mkuu wa wilaya ya Ifakara Wakili Dunstan Kyobya wakati wa  uzinduzi wa Jukwaa la Jikubali lililofayika katika viwanja vya shule ya Sekondari ya wasichana ya Ifakara na kusisitiza vijana waliopo katika kundi hilo wapo hatarini hususani watoto wakike.


“Nitoe wito kwa waalimu na wahudumu wa afya wa ngazi zote kufanya ufuatiliaji wa karibu kwa wanafunzi ili kubaini mwenendo wa tabia zao na kuwaelimisha, hili liendane sambamba na kuendelea kuimarisha mawasiliano kati ya walimu na wanafunzi, walimu na wazazi ili kujenga utaratibu wa kuwa karibu na vijana wetu” amesema Kyobya


Wakili Kyobya amesema tafiti zinaonyesha katika kila asilimia 100 ya maambukizi mapya asilimia 38 huwa ni kundi la miaka15- 24 huku watoto wa kike wakiwa hatarini zaidi.


“ASILIMIA 38 ya hali ya maambukizi mapya ya VVU  ni vijana wenye umri wa miaka 15-24 (yaani katika kila watu 10 wanaopata maambukizo mapya ya VVU wanne ni vijana wa umri huu). ambapo katika kundi hili ASILIMIA 80 ni wasichana, sasa tuanze kujenga utaratibu maafisa elimu muweke muda walau kwa mwezi mara moja wawe wanakutana na wataalamu kuja kuzungumza”. Amesema Wakili Kyobya


Kwa upande wake Mkurugenzi  wa mji  wa Ifakara Lena Nkae ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wanafunzi kutojiskikia upweke pale wanapoamua kukabiliana na vishawishi na wao kama wilaya watahakikisha wanaitekeleza kwa vitendo kampeni ya Jikubali.


“Wanafunzi wote kwa ujumla msiwe wa pweke, wazazi  wamewalea na kuwakabidhi kwa walimu tuwasikilze walimu na tunaomba Kampeni hii tuipokee kwa mikono miwili tuendeleze  kwa shule zote hadi mtaa lengo ni kuahakikisha mnashinda vishawishi na  mnajikubali na kuwa bora” amesema Lena


Nae mmoja wa wanafunzi waliojitokeza kushuhudia uzinduzi wa kampeni ya Jikubali wilayani hapo Nuphaiya Kusi ambaye ni mwanafunzi wa kidato sita katika shule ya wasichana Ifakara amesema vijana walio katika umri balehe, wataanza kuhamasisha makundi hayo kujikinga na tabia hatarishi zinazosababisha maambukizi ya VVU na mimba za utotoni kupitia jukwaa la kampeni ya mabadiliko ya tabia JIKUBALI