Customer Feedback Centre

Ministry of Health

HAKIKISHENI MNATEKELEZA MAELEKEZO YA SERIKALI - DKT. JINGU

Posted on: August 2nd, 2024



Na WAF - DAR ES SALAAM

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu amewataka Wakuu wa Hospitali za Kanda, Maalumu na za Taifa pamoja baadhi ya Wakurugenzi wa Wizara ya Afya kutekeleza maelekezo ya serikali ya kuhakikisha mifumo ya TEHAMA inayotumika katika taasisi inasomana na mifumo mingine ya Serikali.

Dkt. Jingu amesema hayo Leo Agosti 2, 2024 amefanya kikao na Wakuu wa Hospitali za Kanda, Maalumu na za Taifa pamoja baadhi ya Wakurugenzi wa Wizara ya Afya kikao kilichofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara ya Afya (NIMR) Jijini Dar es Salaam,

Amesema maelekezo hayo yanakuja kipindi ambapo serikali inazidi kusisitiza uboreshaji wa huduma za Afya na kuhakikisha huduma za Afya zinakuwa bora katika ngazi zote za Afya.

Katika kutekeleza maelekezo haya, ameelekeza kwamba utekelezaji uende sambamba na utumiaji wa mfumo wa tiba mtandao ambao Serikali imeshauweka katika Hospitali za ngazi ya mikoa ili kuboresha huduma.

Dkt Jingu ameongeza lengo ya jitihada zote za Serikali ni kupunguza adha za kupata huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kwa wananchi, ambapo uimara wa mifumo hiyo utachangia kupunguza rufaa za nje ya nchi kwa watanzania.

Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe, Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wizara ya Afya Issa Ng’imba, Mkurugenzi wa idara ya Tiba Dkt. Hamad Nyembea Mkurugenzi wa kitengo cha TEHAMA Wizara ya Afya Silvanus Ilomo Wizara ya Afya na baadhi ya wakurugenzi na Taasisi akiwemo Dkt. Peter Kisenge Mkurugenzi Taasisi ya Moyo ya Jakaya kikwete, Prof. Abel Makubi kutoka Hospitali ya Benjamini Mkapa na wengineo.