Customer Feedback Centre

Ministry of Health

ELIMU INAHITAJIKA ZAIDI KWA VIJANA ILI KUJIKINGA NA MAAMBUKIZI YA VVU

Posted on: August 19th, 2024

Na WAF - Dodoma 


Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Afya na masuala ya UKIMWI Mhe. Elibariki Kingu ameiagiza Wizara ya Afya kuendelea kutoa elimu hasa kwa kundi la vijana rika balehe ili kupata uelewa wa kujikinga na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI. 


Mhe. Kingu ametoa maelekezo hayo leo Agosti 19, 2024 mbele ya Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama pamoja na Naibu Waziri Dkt. Godwin Mollel wakati wa kikao cha kamati ya kudumu ya Afya na masuala ya UKIMWI kilichofanyika katika kumbi za Bunge Jijini Dodoma. 


"Mbali na utolewaji wa elimu lakini pia Wizara ihakikishe inakuwa na taarifa sahihi zenye kuonesha idadi ya walio tibiwa, walio kufa na UKIMWI, na waliopona magonjwa ya Homa ya Ini na magonjwa mengine." Amesema Mheshimiwa Kingu


Maelekezo mengine aliyoyatoa Mhe. Kingu ni pamoja na kuweka mikakati ya kutunisha mfuko wa Afya ili kuendeleza mapambana ya kutokomeza UKIMWI, kuwepo mfumo wa EHMS ambao utasaidia kupunguza changamoto nyingi zikiwezo za mfuko wa Bima ya Afya (NHIF). 


Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya itaendelea kuweka mkazo wa utoaji wa elimu VVU hasa kwa vijana, hali itakayosaidia kujikinga na maambukizi ya UKIMWI na kupelekea kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa huo na kuutokomeza kabisa. 


"Vijana wengi wa kike wana uhusiano na watu wazima, vilevile wana uhusiano na vijana wenzao wakitoka huku wana kwenda huku hivyo kama wamepata maambukizi kwa watu wazima wanayapeleka kwa vijana wenzao." Amesema Waziri Mhagama


Nae, Mkuu wa Programu Wizara ya Afya Dkt. Catherine Joachim awali wakati akiwasilisha Taarifa ya utekelezaji kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Juni 2024 ya mpango wa Taifa wa kudhibiti UKIMWI, magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini (NASHCoP) amesema Serikali imeendelea kupanua huduma za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa kujumuisha huduma za kuzuia maambukizi ya Kaswende na Virusi vya homa ya ini aina ‘B’. 


"Takwimu zinaonesha, jumla ya vituo 7,830 sawa na 96% ya vituo 8,164 vinavyotoa huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto viliweza kutoa huduma za kuzuia maambukizi ya VVU na Kaswende kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, ikilinganishwa na vituo 7,386 sawa na 99% kati ya 7,428 vilivyotoa huduma hizo kwa mwaka 2022 ambalo ni ongezeko la 3%, ikiendana na ungezeko la vituo vya huduma ya Afya za msingi." Amesema Dkt. Catherine