Customer Feedback Centre

Ministry of Health

BILIONI 561 KUSHUGHULIKIA CHANGAMOTO UZALISHAJI BIDHAA ZA AFYA

Posted on: August 20th, 2024

Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Afya na masuala ya UKIMWI Mhe. Elibariki Kingu ameishauri Wizara ya Afya kuendelea kuisimamia Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kwa kuipatia mtaji wa Bilioni 561.5 ili kukabiliana na changamoto za uzalishaji na uendelezaji wa viwanda vya dawa, vifaa na vifaa tiba ili kurahisisha upatikanaji wa bidhaa hizo kwa wananchi. 


Mhe. Kingu amesema hayo leo Agasti 20, 2024 kwenye kikao cha kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI baada ya Wizara ya Afya kuwasilisha taarifa ya utendaji wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) pamoja na taarifa ya mikakati ya kukabiliana na changamoto ya Afya ya Akili nchini.


 “Viwanda vya dawa, vifaa na vifaa tiba vinatakiwa kuendelezwa kwa kupatiwa mtaji wa kutosha ili kukabiliana na changamoto kama vile gharama kubwa za nishati pamoja na rasilimali watu.”Amasema Mhe. Kingu


Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imepokea maelekezo ya kamati na Wizara imejipanga kupunguza gharama za uzalishaji katika viwanda vya dawa, vifaa na vifaa tiba ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa nyingi zenye ubora pamoja na kuboresha huduma za afya 


“Gharama za uzalishaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba zimekua kubwa kutokana na ongezeko la Nishati za uzalishaji pamoja na rasilimali watu, hivyo kuwa na mbinu mbadala katika kupunguza gharama hizo ikiwa ni pamoja na kutumia gesi katika uzalishaji pamoja na vifaa saidizi.”Amesema Waziri Mhagama 


Katika hatua nyingine Waziri Mhagama amesema, Serikali imerudisha Diploma ya Uuguzi ya Afya ya Akili pamoja na 'Clinical Offices' ambayo itaongeza ufanishi kwa utoaji wa huduma kwa wagonjwa wa Afya ya Akili maana changamoto hii imekua ikiongezeka kutokana na mtindo wa maisha.


Awali Wakati akiwasilisha taarifa ya mikakati ya kukabiliana na changamoto ya Afya ya Akili, Mkururenzi Msaidizi wa Magonjwa Yasiyoambukiza Dkt. Omari Ubuguyu amesema Serikali imewezesha ujenzi na ukarabati wa majengo ya kliniki za methadone Zaidi ya 16 zenye gharama zaidi ya Bilioni 5.  


"Hospitali Taifa ya Afya ya Akili Mirembe imewezeshwa kupata Zaidi ya shilingi Bilioni 4 katika kipindi cha miaka 5 iliyopita ili kuweza kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma katika hospitali hiyo." Amesema Dkt. Ubuguyus