BILIONI 145 KUCHANGWA NA WADAU, MFUKO WA AFYA WA PAMOJA
Posted on: July 1st, 2024
.
Na WAF, Dar Es Salaam
Serikali kupitia Wizara ya Afya inatarajia kupokea bilioni 145 kwa mwaka wa fedha 2024/25 kutoka bilioni 126 mwaka 2023/24 ongezeko la asilimia 15, kutoka kwa wadau wanaochangia sekta ya afya kupitia mfuko wa afya wa pamoja (Health Basket Fund)
Hayo yamesemwa leo Julai Mosi, 2024 na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu wakati wa kikao kazi cha kuridhia mpango kazi na matumizi ya fedha zinazotolewa kupitia mfuko wa pamoja wa afya zikiwemo Balozi na Benki ya Dunia kwa mwaka wa fedha 2024/25.
Dkt. Jingu amesema fedha hizo zitagawanywa kwenye Halmashauri shilingi bilioni 130.1, Wizara ya Afya bilioni 5.9, Mikoa bilioni 5.9 na bilioni 2.9 zitakwenda Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Aidha, ameongeza kuwa lengo la Mchango wa mfuko wa afya wa pamoja kutoka kwa wadau hao ni kuimarisha Huduma za Afya katika ngazi ya msingi hususani kwenye ununuzi wa vifaa tiba, dawa na kuimarisha huduma za Chanjo.
“Mbali na maeneo hayo pia fedha hizo zitatumika kuimarisha huduma za mama na mtoto pamoja na uendeshaji wa vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya msingi vipatavyo 6214”.
Kwa upande wake Mratibu wa Kamati ya washirika wa maendeleo wa mfuko wa Afya wa pamoja kutoka ubalozi wa Uswiss, Bi. Jacqueline Matoro ameipongeza serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya kwa kuhakikisha inaimarisha huduma za Afya na upatikanaji wake kuanzia ngazi ya msingi na kushukuru kwa ushirikiano Wizara ya Afya inaoutoa kwa wadau wa maendeleo katika sekta ya Afya.
Mfuko wa Afya wa pamoja ulianzishwa mwaka 1999 ambapo hadi sasa umeendelea kuunga mkono juhudi za serikali ambapo wadau hao ni Serikali ya Canada, Switzerland, Ireland, World Bank, UNICEF, UNFPA, KOICA, Danida Investment pamoja na mdau mpya Serikali ya Uingereza.