ASILIMIA 14 YA FEDHA ZA BIMA YA AFYA KWA WOTE KUGHARAMIA MAGONJWA SUGU
Posted on: August 12th, 2026Na Hassan Kimweri, WAF – Dodoma
Asilimia 14 ya fedha zinazotengwa kupitia Bima ya Afya kwa Wote zitaelekezwa katika kugharamia matibabu ya wananchi wenye magonjwa sugu, ikiwa ni hatua ya kuhakikisha wagonjwa wanaohitaji matibabu ya muda mrefu wanapata huduma bila kikwazo cha kifedha.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe amesema hayo leo Agost 12, 2026 wakati akijibu maswali ya Wabunge kuhusu utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI mkoani Dodoma.
"Utaratibu huu umeainishwa katika Sheria ya Bima ya Afya na unalenga kuhakikisha wananchi wenye magonjwa sugu wanapata huduma wanazohitaji, hususan wale wasio na uwezo wa kugharamia matibabu hayo," amesema Dkt. Magembe
Aidha, Dkt. Magembe amesema utekelezaji wa utaratibu huo unaenda sambamba na juhudi nyingine za Serikali za kutenga Shilingi bilioni tano kila mwaka kwa ajili ya matibabu ya ubingwa bobezi, kuimarisha huduma za rufaa ili kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma katika ngazi inayostahili na kuboresha matumizi ya mifumo ya TEHAMA kwa lengo la kudhibiti ubadhirifu na kuongeza ufanisi.
Amesema, Bima ya Afya kwa Wote inalenga kuongeza upatikanaji wa huduma za afya, uwezo wa wananchi kumudu gharama za matibabu na kuhakikisha huduma zinazotolewa zina ubora unaostahili kwa kila mwananchi.
Mwisho, Dkt. Magembe amesema pamoja na kugharamia matibabu, Serikali imeendelea kuweka mkazo katika kinga na udhibiti wa magonjwa, hususan magonjwa yasiyo ya kuambukiza ili kupunguza idadi ya wananchi wanaohitaji huduma za matibabu na hivyo kulinda uendelevu wa mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote.