Customer Feedback Centre

Ministry of Health

ACHENI KUFANYA KAZI KWA MAZOEA, TUNATAKA UBORA WA HUDUMA KWA WANANCHI", DKT MOLLEL

Posted on: November 17th, 2023

"

NA.WAF, Dar es Salaam 

Naibu Waziri wa Afya Dkt Godwin Mollel amewataka Waganga wafawidhi wa Hospitali zote nchini kuwajibika na kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili kuleta tija ya uwekezaji uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan katika sekta ya afya.


Dkt. Molel ametoa kauli hiyo leo alipofanya ziara katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kuangalia hali ya utoaji huduma za afya na kufanya mazungumzo na Wakuu wa Taasisi za Afya ikiwemo Hospitali ya taifa ya Muhimbili (MNH), Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Mifupa MOI, Bohari ya Dawa (MSD), Shirika la Bima la taifa NHIF, Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA), Mganga Mkuu wa mkoa pamoja na Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Rufaa za mkoa wa Dar es saalam .


Dkt. Mollel amesema Serikali haitamvumilia kiongozi yoyote anayekwamisha juhudi za uboreshaji wa huduma katika sekta ya afya nchini kwani Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mapinduzi makubwa katika sekta ya afya hivyo ni jukumu la usimamizi imara ili kuleta ubora wa Huduma kwa wananchi 


Aidha, Naibu Waziri wa Afya ameeleza mafanikio katika uboreshaji wa huduma sio uwekezaji wa vifaa tiba na rasilimali watu pekee bali ni pamoja na kuwepo kwa uongozi bora na kila mmoja kutimiza wajibu wake.


“Mhe. Rais wa Awamu ya Sita Dkt.Samia Suluhu Hassan ameshamaliza kazi yake kwa kuwekeza Trilioni 6.7 katika miundombinu, taaluma, teknolojia tiba na rasilimali watu sasa ni wakati wa kila kiongozi kutekeleza majukumu yake kwakua sera ya Wizara ya Afya kwasasa ni kuhakikisha Hospitali za Serikali zinatoa huduma bora zinazokidhi viwango”. Amesema Dkt. Mollel


Dkt. Mollel amesema ziara yake ni kutokana na agizo la Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kutembelea hospitali zote nchini juu ya kuangalia ubora wa huduma za afya kwa wananchi.


“Mhe. Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ameniagiza kutembelea hospitali zote nchini kuangalia suala la ubora katika utoaji huduma na kufanya marekebisho katika maeneo ambayo hayafanyi vizuri, kiongozi kama hutekelezi majukumu yako inavyotakiwa unapaswa kujitafakari, hata hivyo napenda kuzipongeza Taasisi za MNH, MOI na JKCI kwa kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya afya”. Amesisitiza Dkt. Mollel


Wakati huohuo Dkt. Mollel amesema Wizara ya Afya imedhamiria kuhakikisha kuwa mifumo ya TEHAMA katika hospitali kuanzia ngazi ya zahanati hadi taifa inasomana ili kumpunguzia muda mgonjwa wa kusubiri kupata matibabu kwa kurudia kufanya kipimo isipokua pale inapolazimu kurudia kufanya kipimo husika.