Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WELEDI NA UMAKINI UNATAKIWA KWENYE UCHUKUAJI WA SAMPULI ZA MAJI - MWAKITALIMA

Posted on: July 17th, 2025

Na WAF, Morogoro 


Wataalamu wa afya ya mazingira kutoka halmashauri mbalimbali nchini wametakiwa kuzingatia weledi na mafunzo waliopatiwa wakati wa uchukuaji wa sampuli za maji kwa ajili ya vipimo, ili kubaini usalama wa maji ya kunywa na kuzuia magonjwa ya mlipuko.


Hayo yamebainishwa na leo Julai 17, 2025  mkoani Morogoro na Mkuu wa Sehemu ya Chakula Salama, Maji Salama na Usafi wa Mazingira kutoka Wizara ya Afya, Bw. Anyitike Mwakitalima, wakati wa mafunzo ya vitendo kuhusu usalama wa maji ya kunywa.


“Wataalamu hakikisheni mnatumia kwa usahihi kila hatua mliyojifunza kabla ya kwenda kuchukua sampuli kwenye maeneo husika na  kupata matokeo sahihi, yanayokubalika kitaalamu kwa hatma ya afya za watanzania, amesema Bw. Anyitike Mwakitalima 


Naye, Afisa afya Mwandamizi mtaalam wa Epidemologia Bw. Ambakisye Mchiche amebainisha kuwa kufanya kwa vitendo kunatoa wepesi wa kuelewa mafunzo hayo na kutimiza dhima yake ya kuhakikisha usalama wa maji ya kunywa kwa wananchi unakuwa mkubwa


Amesema sampuli zilizochukuliwa kutoka mfereji, mito, visima virefu, visima vifupi na maji ya bomba ni kwa lengo la kuweka uhakiki na kutofautisha matokeo ili iwe rahisi kwa wataalam wanaopata mafunzo kuona tofauti baina ya maji yaliyo salama na ambayo hayafai kwa matumizi ya kunywa


"Utekelezaji wa mafunzo kwa njia ya vitendo hurahisisha uelewa wa dhana nzima, sambamba na kutimiza lengo la kuhakikisha maji ya kunywa kwa wananchi yanakuwa salama." Amesema Bw.Ambakisye Mchiche


Mafunzo ya vitendo kwa uchukuaji na upimaji wa sampuli za maji yameonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata huduma bora ya maji salama, huku wataalam wakiwekwa mstari wa mbele ili kulinda afya ya jamii kwa kupewa elimu kuhusu mbinu bora za uchunguzi wa maji, viashiria vya uchafuzi, na matumizi ya vifaa vya kisasa vya kupima ubora wa maji, kama sehemu ya afua ya kitaifa wa kupambana na magonjwa yanayotokana na maji machafu.