Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI, WHO ZAJIIMARISHA KUKABILI DHARURA ZA AFYA

Posted on: December 17th, 2025

NA WAF, Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuimarisha jitihada za pamoja kwa kushirikiana na Wizara za Kisekta pamoja na wadau mbalimbali, ikiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO), katika kukabiliana na dharura za kiafya.

Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 16 Oktoba, 2025 Jijini Dodoma, na Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya Timu za Matibabu ya Dharura (Emergency Medical Teams – EMTs), yaliyoratibiwa na Wizara ya Afya kwa ufadhili wa WHO kupitia mradi wa Pandemic Fund.

“WHO wamekuwa wadau wakubwa katika kukabiliana na dharura na tumepiga hatua kubwa sana. Tuna sababu ya kuweka nguvu ya pamoja kuendelea kukabiliana na dharura, hususan kutokana na mabadiliko ya tabianchi, milipuko ya magonjwa na ajali,” amesema Dkt. Magembe.

Aidha, Dkt. Magembe amesema kuwa uwepo wa Dawati la Afya Moja umechangia kwa kiwango kikubwa katika kuimarisha uratibu na ufanisi wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

“Wenzetu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na Jeshi la Polisi tunafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa. Tunapozungumzia dharura, tunazungumzia masuala mbalimbali ikiwemo magonjwa ya mlipuko na ajali, hivyo kushikamana ni jambo muhimu sana,” ameongeza.

Kwa upande wake, Mtaalamu wa Afya ya Jamii kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Dkt. Jerry Jonas, amesema WHO imekuwa ikishirikiana bega kwa bega na Tanzania katika masuala ya afya ikiwemo dharura za afya, hivyo mafunzo hayo yatakuwa na mchango mkubwa katika kujiweka tayari kukabiliana na dharura.

Naye Mkurugenzi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Makame Khatib Makame, amesema mafunzo hayo ni muhimu katika kuimarisha timu za dharura za kukabiliana na maafa.

“Tunaishukuru Wizara ya Afya kwa kuweka nguvu za pamoja katika kuandaa mafunzo haya ambayo yanaongeza msukumo katika shughuli za uokozi wakati wa dharura,” amesema.