WATAALAM WA MAABARA WATAKIWA KUSIMAMIA WELEDI NA MATUMIZI SAHIHI YA RASILIMALI
Posted on: December 20th, 2025NA WAF, Dar es Salaam
Wataalam wa maabara wametakiwa kusimamia weledi katika utekelezaji wa majukumu yao pamoja na kuhakikisha matumizi sahihi ya rasilimali ili kuboresha utoaji wa huduma bora za afya kwa jamii.
Wito huo umetolewa leo, Desemba 19, 2025, na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Afya Bw. Issa Ng’imba wakati wa mahafali ya mafunzo ya Global Laboratory Leadership Program (GLLP) yaliyofanyika jijini Dar es Salaam
Bw. Ng’imba amesema mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo viongozi chipukizi wa maabara katika masuala ya uongozi na kuwapa mbinu za kukabiliana na changamoto zinazowakabili katika maeneo yao ya kazi.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yamekuja kwa wakati muafaka, hasa katika kipindi ambacho kuna hitaji la kuimarisha mifumo ya maabara, hususan katika masuala ya utawala, utatuzi wa kero za wagonjwa, upimaji pamoja na ushiriki katika ufuatiliaji wa magonjwa.
“Niishukuru Serikali pamoja na mdau wetu, Global Fund, kwa kutambua umuhimu wa kuwezesha upatikanaji wa viongozi chipukizi katika fani ya maabara nchini,” amesema Bw. Ng’imba.
Aidha, ameomba utaalamu uliopatikana kupitia mafunzo hayo usiishie kwa wahitimu pekee, bali utumike pia kuandaa na kufundisha kozi hiyo katika vyuo vingine kwa gharama nafuu ili kuwafikia wataalam wengi zaidi wa maabara wenye uwezo wa uongozi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Huduma za Maabara kutoka Wizara ya Afya, Bw. Reuben Mkala, amesema kuwa ubora wa huduma za maabara ni mhimili muhimu katika kuboresha huduma za afya kwa ujumla, hasa katika utambuzi wa magonjwa na upatikanaji wa takwimu sahihi.
Naye, Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Mfuko wa Dunia (Global Fund), Hussein Athuman, amesema shirika hilo litaendelea kuunga mkono jitihada za kuimarisha rasilimali watu kupitia utoaji wa msaada wa kitaalamu.