Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI YAAHIDI KUONGEZA WIGO WA UTOAJI HUDUMA ZA AFYA

Posted on: July 13th, 2025

Na WAF, Dodoma 


Naibu Waziri ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya Afya Dkt. Festo Dugange, amesema Serikali itaendelea kuongeza wigo wa utoaji na upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi huku akiwasisitiza watoa huduma za afya kuwa wabunifu na kuendelea kuwajibika kwa wananchi.


Dkt. Dugange  amesema hayo leo Julai 13, 2025 wakati  akikufunga Mkutano Mkuu wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri  uliofanyika jijini Dodoma katika ukumbi wa mikutano wa wa Jakaya Kikwete.


Dkt. Dugange amesema kwa mwaka wa fedha 2025/26 Serikali itajenga hospitali 43 za Halmashauri, pia itanunua vifaa tiba kwajili ya hospitali 142 sambamba na kujenga zahanati 184.


"Kupitia vyanzo vya ndani vya Halmashauri Serikali imepanga kutekeleza miradi mbali mbali ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya 28, ukamilishaji wa vituo vya afya 74 pamoja na ujenzi wa zahanati 32 pamoja na ukamilishaji wa zahanati 325" amesema Dkt. Dugange.


Katika hatua nyingine Dkt. Dugange amesema ni muhimu kuwa na sanduku la maoni ili kupata mrejesho na changamoto za wanachi ili ziweze  kupatiwa ufumbuzi.


"Nawaagiza waganga wakuu wa Halmshauri na mikoa kuendelea kusikiliza kero za wananchi kuhusiana na Afya pia kwenye kila kituo cha Afya au Zahanati ni lazima kuwe na sanduku la maoni, " amesema Dkt. Dugange.


Akihitimisha Mkutano huo, Dkt. Dugange amewataka watumishu wa Afya kuendelea kubuni mbinu za kibunifu ili kukidhi mahitaji ya wananchi pamoja na kuzingatia maadili ya kazi yao.


Wizara ya Afya kwa ushirikiano na Ofisi ya Rais TAMISEMI iliandaa Mkutano wa siku kwa ajili ya Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kujadiliana na kuweka mikakati ya kuboresha sekta ya afya nchini na utoaji huduma kwa muda wa siku mbili.