Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

ZAIDI YA WANANCHI 3,000 KUPATIWA MATIBABU KAMBI YA MADAKTARI BINGWA TABORA.

Posted on: May 6th, 2025

NA WAF - TABORA.

Zaidi ya wagonjwa 3,000 wanatarajiwa kupata matibabu kwenye kambi ya madaktari bingwa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi ambazo zitajumuisha uchunguzi, vipimo na matibabu mbalimbali yanayotolewa na wataalam bingwa katika maeneo yaliyolengwa.

Hayo yamebainishwa leo Mei 5, 2025 na Katibu Tawala wa Mkoa wa, Dkt. John Mboya katika ufunguzi wa kambi ya madaktari bingwa na ubingwa bobezi wa Rais Samia, katika Hospitali ya Rufaa ya kitete, mkoa wa Tabora.

Dkt. Mboya ameeleza manufaa yanayopatikana kwa wananchi kutokana na uwepo wa huduma hizo za kibingwa ikiwepo kutosafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo pamoja na kuongeza ujuzi kwa madaktari waliopo katika hospitali hiyo.

“Tunatoa shukurani za dhati kwa Serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya utoaji wa huduma za afya kwa kupeleka fedha za ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za Afya pamoja na manunuzi ya vifaa tiba,” amesema Dkt. Mboya.

Aidha, Dkt. Mboya amewaomba wananchi wote wenye matatizo ya kiafya kuhudhuria kwenye kambi hiyo ili kuonana na kutibiwa na madaktari bingwa na bingwa bobezi ili kuwapunguzia gharama za kusafiri umbali mrefu nje ya mkoa huo kufuata huduma.

Kwa upande wake Mkazi wa Tabora, Recho Mbinda ameishukuru Serikali kwa kufikisha huduma hizo ambazo awali walikuwa wakitumia gharama kusafiri kwenda maeneo mbalimbali nchini.

Kambi ya Matibabu ya Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi wa Rais Samia imeanza leo Mei 5, 2025 na itamalizika Mei 9, 2025.