Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WIZARA YA AFYA YATOA ELIMU KWA WANAHABARI JUU YA UKOMA

Posted on: January 27th, 2024

Katika kuelekea maadhimisho ya siku ya  Ukoma dunia Serikali kupita Wizara ya Afya imetoa elimu juu ya  kuthibiti ugonjwa wa Ukoma kwa Waandishi wa Habari.

Elimu hiyo imetolewa leo tarehe 27 Januari, 2024 Dodoma na Mratibu wa mpango wa Taifa wa kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma Wizara ya Afya Dkt. Deusi Kamara wakati wa akizungumza na waandishi wa habari.

Dkt. Kamara amesema ugonjwa wa Ukoma unasababishwa na bakteria aitwae Mycobacterium Leprae na unaambukizwa kwa njia ya hewa hivyo jamii kuacha dhana potofu juu ya ugonjwa huo.

“Vimelea vya ugonjwa wa ukoma vinaambukiza kwa njia ya hewa, endapo mtu mwenye vimelea vya ugonjwa huu akakohoa au kupiga chafya bila kuziba mdomo basi anaweza kumuambukiza mtu mwingine ivyo tuachane na dhana potofu za kusema mtu mwenye ugonjwa huu analaana au amerogwa” Amesema Dkt. Kamara.

Amesema dalili za ugonjwa wa Ukoma ni mtu kupata mabaka yenye rangi ya shaba ambayo hayawasi wala kuuma na kuvimba kwa mishipa ya fahamu kwa sababu ya vimelea vya ugonjwa huo kupenda kuzalia kwenye mishipa ya fahamu.

“nitoe wito kwa jamii pindi unapoona dalili kama hizi au mabadiliko yoyote kwenye ngozi yako, kama ni mabaka, vipele au uvimbe ni vyema kuwahi katika kituo cha kutolea huduma za Afya ili unapogundulika umepata maambukizi ya ugonjwa huu kuanza tiba mara moja kwa sababu ukoma unatibika na tiba zake kutolewa bure kwenye vituo vya Afya kote nchini”. Amesema

Pia Dkt. Kamara amewataka waandishi wa habari kutumia vizuri vipawa vyao katika kusambaza elimu na hamasa kwa jamii dhidi ya mapambano ya kutokomeza unyanyapaa dhidi ya waathirika wa ukoma.

Ugonjwa wa Ukoma uadhimishwa kila ifikapo tarehe 28 Januari ya kila mwaka Duniani ambapo kitaifa mwaka huu yanakwenda na kauli mbiu “Thamini Utu; Tokomeza Unyanyapaa dhidi ya Waathirika wa Ukoma