Wizara Ya Afya

WIZARA YA AFYA YAHIMIZA WATAALAMU WA AFYA MAGEREZA KUCHANGAMKIA FURSA ZA MASOMO

Posted on: October 21st, 2026

Na Aisha Swahibu, WAF – Dodoma

Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Bruno Sunguya, amewataka wataalamu wa afya wa Jeshi la Magereza nchini kuchangamkia fursa za masomo zinazofadhiliwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya, ikiwemo ile ya Samia Scholarship, ili kuongeza ujuzi, weledi na uwezo wa kutoa huduma bora za afya kwa wananchi.

Prof. Sunguya ametoa rai hiyo leo Oktoba 21, 2026, jijini Dodoma kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Wataalamu wa Afya wa Jeshi la Magereza, amesisitiza umuhimu wa wataalamu hao kutumia fursa za mafunzo na kubadilishana uzoefu ili kuendana na mabadiliko ya sayansi, teknolojia na mahitaji ya huduma za afya.

Amesema Serikali inaendelea kuweka mkazo wa uwekezaji wa rasilimali watu wenye weledi, utu na uwezo wa kutoa huduma jumuishi, hatua inayokwenda sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utalii wa tiba kwa kuimarisha huduma za kibingwa na bobezi nchini.

Prof. Sunguya amesema Wizara ya Afya iko tayari kushirikiana na Jeshi la Magereza katika mafunzo na kubadilishana uzoefu kwa kadri fursa zitakavyopatikana, ili kuimarisha uwezo wa wataalamu na kuboresha huduma zinazotolewa katika vituo vya afya vya Jeshi hilo.

Amewapongeza wataalamu wa afya wa Jeshi la Magereza kwa kazi wanayoifanya ya kuhudumia makundi mbalimbali, akisisitiza kuwa Serikali inatambua mchango wao na itaendelea kushirikiana na Jeshi hilo katika kuboresha huduma za afya kwa kuzingatia miongozo na viwango vinavyotakiwa.

Katika hatua nyingine, Prof. Sunguya ameipongeza Serikali kupitia uongozi wa Jeshi la Magereza kwa jitihada za kuboresha miundombinu ya afya, ikiwemo ujenzi na ukarabati wa vituo vya kutolea huduma hizo. Ametaja ujenzi wa Hospitali ya Kanda ya Msalato kuwa ni hatua muhimu inayotarajiwa kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za afya kwa wafungwa, mahabusu, watumishi wa Jeshi hilo na wananchi wa Kata za Msalato na Makotupora wenye wakazi zaidi ya 28,000.