Wizara Ya Afya

WIZARA YA AFYA, JESHI LA MAGEREZA KUSHIRIKIANA KUKAMILISHA HOSPITALI YA KIMKAKATI MSALATO

Posted on: October 21st, 2026

Na Aisha Swahibu, WAF – Dodoma

Wizara ya Afya imeahidi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Magereza katika kuharakisha ukamilishaji wa hospitali ya kimkakati inayojengwa eneo la Msalato, jijini Dodoma, ikiwemo kushughulikia changamoto za upatikanaji wa vifaa tiba ili kuiwezesha kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Ahadi hiyo imetolewa leo Oktoba 21, 2026 na Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Bruno Sunguya, wakati alipotembelea eneo la ujenzi wa hospitali hiyo kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi na kujadiliana na viongozi wa Jeshi la Magereza kuhusu hatua zinazohitajika ili kukamilisha mradi huo.

Amesema tathmini ya awali imeonesha kuwa majengo ya hospitali hiyo yana ubora unaokidhi vigezo vya ujenzi wa majengo ya kutolea huduma za afya, huku baadhi ya majengo yakiwa yamekamilika na mengine yakifikia hatua za mwisho za ujenzi.

Prof. Sunguya ametaja majengo yaliyotembelewa kuwa ni pamoja na jengo la upasuaji, jengo la huduma za mama na mtoto pamoja na jengo la maabara, ambayo ni sehemu muhimu katika kuhakikisha hospitali hiyo inakuwa na uwezo wa kutoa huduma za afya kwa ufanisi.

Profesa Sunguya amesema eneo la Msalato lina umuhimu mkubwa wa kimkakati kutokana na ukubwa wake, ukaribu na barabara kuu pamoja na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato unaojengwa, hali inayotoa fursa ya kuliendeleza zaidi kwa shughuli mbalimbali za sekta ya afya.

Ameeleza kuwa, pamoja na kuhudumia Jeshi la Magereza na jamii inayozunguka eneo hilo, hospitali hiyo inaweza kuwa na umuhimu mpana katika kuimarisha uwezo wa kukabiliana na majanga ya ajali milipuko ya magonjwa na changamoto nyingine za kiafya, kulingana na mahitaji ya Taifa.

Aidha, Prof. Sunguya amesema Wizara ya Afya itaendelea kushirikiana na Jeshi la Magereza pamoja na wadau wengine wa Serikali, wakiwemo viongozi wa mikoa na Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kuhakikisha changamoto zinazokwamisha ukamilishaji wa hospitali hiyo zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.