Wizara Ya Afya

WAZIRI MCHENGERWA AITAKA BODI YA WADHAMINI MUHIMBILI KUSIMAMIA UJENZI WA MUHIMBILI MPYA

Posted on: September 30th, 2026

Na Clement Robert, WAF - Dar es Salaam

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, ameitaka Bodi mpya ya Wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili kuhakikisha mradi wa ujenzi wa Muhimbili Mpya unaanza na kusimamiwa kikamilifu, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuwa na Hospitali yenye sura mpya ya Karne ya 21.

Waziri Mchengerwa ametoa agizo hilo leo Septemba 30, 2026 wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili na miradi minne ya kimkakati katika hospitali hiyo, Mkoani Dar es salaam.

Amesema mradi wa Muhimbili Mpya ni wa kimkakati na wa kihistoria, hivyo unapaswa kupewa kipaumbele katika majukumu ya kawaida ya Bodi ili utekelezaji wake uende sambamba na mpango kazi uliowekwa.

Amebainisha kuwa Serikali inalenga kuona Muhimbili yenye mwonekano wa Karne ya 21 unaoendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, huku huduma zake zikiendelea kuimarika kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Mhe. Mchengerwa amesema Muhimbili ina nafasi ya kipekee kama kituo cha mwisho cha rufaa nchini na inapaswa kujipambanua kwa huduma za kibobezi za hadhi ya kimataifa, zitakazosaidia kupunguza sababu za Watanzania kutafuta matibabu nje ya nchi.

Ameitaka Bodi hiyo kufanya kazi kwa karibu na Menejimenti ya Hospitali, ikiongoza kwa maono na kusimamia utekelezaji kwa uthabiti, huku Wizara ya Afya ikiendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kufikia Muhimbili Mpya inayokusudiwa.