WANANCHI WENGI BADO HAWANA MWITIKIO WA KUPIMA SARATANI
Posted on: October 21st, 2023
Na. WAF - Dar es Salaam
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ameeleza kuwa Watanzania wengi bado hawana mwitikio wa kupima Saratani ambapo amebainisha kuwa kwa mwaka ni asilimia 38 tu ya wagonjwa wa Saratani ndio wanafika katika vituo vya kutoa kutolea huduma za Afya.
Waziri Ummy amesema hayo leo Octoba 21, 2023 baada ya matembezi ya uelimishaji jamii juu ya Saratani yaliyoandaliwa na Ubalozi wa Sweden kwa kushirikiana na Shujaa Cancer Foundation na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Sweden ambapo yaliyoanzia katika Taasisi ya Saratani Ocean Road Jijini Dar es Salaam na kumalizika katika Taasisi hiyo.
“Tunao wagonjwa wengi katika majumba yetu, katika ofisi zetu, katika vijiji vyetu, mitaani kwetu ambao wana Saratani lakini hawajaweza kufika katika hospitali kwa ajili ya huduma za uchunguzi na matibabu hii imekua ni changamoto kubwa”. Amesema Waziri Ummy
Aidha, Waziri Ummy amesema takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa kila mwaka Tanzania ina wagonjwa wapya wa Saratani 42,000 ambapo wagonjwa hao wapya wanaofika kwenye vituo vya huduma za Afya ni takribani 15,900 tu.
Hivyo, amewasisitiza wananchi kujitokeza kupima ugonjwa wa Saratani hususan Saratani ya Matiti kwa ajili ya kujua hali zao mapema na kuanza matibabu kabla haijafika hatua ya Tatu na Nne ya ugonjwa huo.
“Unapofikisha umri wa kusherehekea sherehe yako ya kuzaliwa (Birthday) jipe zawadi ya kwenda kupima Saratani hususan ya Matiti na Mlango wa Kizazi kwa wanawake”. Amesema Waziri Ummy
Amesema, mtu akifikisha miaka 40 anatakiwa kupima Saratani kila baada ya miaka Miwili kwa ajili ya ugunduzi wa awali kwa kuwa Saratani inatibika ikigundulika mapema katika hatua ya kwanza na ya Pili.
Pia, Waziri Ummy amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya itaandaa muongozo kwa mwanamke yeyote mwenye umri wa miaka 30 anaekwenda Hospitali iwe ni Wajibu wa daktari kumuelekeza au kumuelimisha mwanamke huyo kufanya uchunguzi wa kupima Saratani ya Matiti na Saratani ya Mlango wa Kizazi.
“Wakati mgonjwa (mwanamke) akija kupata huduma za Afya katika vituo vyetu tuwe na wajibu wa kuwaelimisha umuhimu wa kupima Saratani ya Matiti na Mlango wa Kizazi kwa kuwa tukiweza kuwagundua mapema wagonjwa wa Saratani basi matibabu yatakuwa rahisi na mgonjwa akigundulika anapona mapema”. Amesema Waziri Ummy
Katika hatua nyingine Waziri Ummy amemshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mashine za Ultrasound hadi katika ngazi za vituo vya Afya, CT-Scan mashine kwenye kila Hospitali ya Rufaa ya Mkoa pamoja na X-Ray kwa lengo la kusogeza huduma bora kwa wananchi.
“Nitumie fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi Serikali yake inavyotekeleza yale yote iliyoyaahidi pia tunaona jinsi Serikali inavyoendelea na juhudi za kuboresha Sekta ya Afya na kuhakikisha huduma za Afya zinakuwa karibu na wananchi ikiwemo huduma za Saratani”. Amesema Waziri Ummy