WANANCHI WAIPONGEZA SERIKALI KUBORESHA MIUNDOMBINU YA AFYA NA HUDUMA BORA
Posted on: March 14th, 2024
Na: WAF, Lindi
Wananchi Wameipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu kwa Maendeleo ya Miundombinu ya Afya na huduma bora katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Hayo yamejiri kufuatilia ziara ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe alipotembelea mikoa ya Mtwara na Lindi kwa ajili ya kukagua miradi ya ujenzi, vifaa, vifaa tiba, ubora wa huduma pamoja na kuongea na watumishi wa sekta ya afya.
Harouni Selemani Harouni akiwakilisha wananchi amesema huduma ambazo zinatolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya zimekuwa nzuri kuanzia mapokezi mpaka kupata huduma wananchi wameonyesha furaha na pongezi kwa serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan kufuatia jitihada zake za kuboresha miundombinu kuleta vifaa vya kisasa kwa ajili ya huduma za afya nchini.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Dkt Grace Magembe amewapongeza watumishi wa afya kwa kutoa huduma bora kwa wananchi na hili limeonekana kwa mwitikio wa wananchi kufuatia upatikanaji wa huduma hasa huduma kwa wateja.
"Wananchi wanapozungumza huwa wanazungumza ya moyoni kabisa, ikiwa mmefanya vibaya watasema mkimfanya vizuri watawapongeza vilevile na nimeona wengi wanawapongeza, sijaona wananchi wakiwasema vibaya sana sana wanazungumzia upungufu ya watumishi ". Amesema Dkt Magembe
Dkt. Grace Magembe amesisitiza umuhimu wa kutoa huduma bora kwa wananchi na kuendelea kutoa huduma bora kwa wateja na kuwahimiza watumishi hao kuzingatia maadili ya kazi na kujituma katika kutoa huduma kwa wananchi.
"Serikali inaendelea kutekeleza ahadi zake za kuboresha sekta ya afya na kuhakikisha kwamba kila mwananchi anapata huduma bora za afya hivyo sisi kama watumishi katika sekta ya afya ni jukumu letu kuwahudumia kwani maboresho aliyofanya Dkt. Samia Suluhu Hassan ni makubwa". Amesema Dkt Magembe