Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

UTOAJI WA HUDUMA ZA MADAKTARI BINGWA WA DKT. SAMIA UMEZINGATIA MAHITAJI YA WAGONJWA

Posted on: May 8th, 2024



Na WAF - NAMTUMBO/TUNDURU.

Mpangilio wa utoaji wa huduma za kibingwa na Ubingwa bobezi wa Madaktari bingwa wa Dkt. Samia katika Hospitali za Halmashauri 184 ikiwemo Halmashauri ya Wialaya ya Namtumbo na Tunduru umezingatia mahitaji ya wagonjwa.

Hali hiyo imebainika Mei 8, 2024 katika Hospitali za Halmashauri za Namtumbo na Tunduru Mkoani Ruvuma ambapo Madaktari bingwa na Bingwa Bobezi wa Dkt. Samia wameanza kutoa huduma za matibabu za Mkoba na kulifikia kila kundi lenye uhitaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi karibu zaidi katika vituo vya Afya ngazi ya msingi.

Wanufaika wa huduma za Mkoba za Madaktari bingwa hao wamesema licha ya huduma za kibingwa kukidhi mahitaji muhimu kwa kutoa huduma ambazo wangelazimika kuzifuata mbali na kwa gharama kubwa lakini pia upatikanaji wa dawa ni mzuri kwani kila dawa watakayoandikiwa na Madaktari Bingwa wanaipata katika Duka la Hospitali.

"Huduma hii kwa ujumla inakidhi mahitaji ya jamii na hasa wagonjwa, wanapokuja Madaktari bingwa kutoka sehemu nyingine wanatusaidia wananchi hasa wa wilaya ya Tunduru, kwa sababu magonjwa ni mengi sasa hivi na madaktari tunao wachache hivyo wanapoongezeka basi huduma inakuwa nzuri na wanatusaidia zaidi wanatunduru na kukidhi mahitaji ya jamii na wahitaji". Aamesema Fidelis Nyakunga mkazi wa Tunduru.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Wilaya ya Namtumbo Dkt. Christopher Obaruni amesema walijiandaa na ugeni huo wa Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia mapema kwa kusogeza huduma karibu n wananchi kwa kuzingatia mahitaji, vitendea kazi na kila watakacho kihitaji katika kuteleza huduma ikiwemo kuagiza dawa za kutosha ili kusaidia wananchi kupata huduma zote hapo.

Nae Kiongozi wa Timu ya Madaktari bingwa wa Dkt. Samia kwa Halmashauri ya Namtumbo ambaye pia ni Daktari bingwa wa Magonjwa ya Watoto Dkt. Maryam Gaitani ameipongeza Serikali, Wizara na OR-TAMISEMI kwa kupanga seti za Madaktari zinazogusa kila kundi la wahitaji wa huduma za kibingwa.