UGONJWA WA KIFAFA UNAONGOZA DUNIANI KATIKA MAGONJWA YA MISHIPA YA FAHAMU
Posted on: February 12th, 2024
Inakadiriwa kuwa takribani watu milioni 50 duniani wana ugonjwa wa kifafa na wengine wapya milioni sita wanagundulika kila mwaka ambapo nchini Tanzania kuna wagonjwa zaidi ya milioni moja wanaokabiliwa na tatizo hilo.
Hayo yameelezwa leo na Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Tumaini Joseph Nagu wakati akizungumza kwenye kongamano la maadhimisho ya siku ya kifafa duniani lililoandaliwa na Chama cha Watalam wa Kifafa Tanzania (TEA) na kuadhimishwa leo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo ameitaka jamii kuacha tabia ya kuwaficha wagonjwa wenye kifafa kwakuwa wagonjwa hawa wakitumia dawa wanaweza kuishi kama watu wengine.
Ameongeza kuwa pamoja na kwamba ugonjwa huu umeanza siku nyingi bado jamii inaendelea kuhusisha na imani potofu na kuwaficha watoto wenye ugonjwa huo ndani na kuwasababisha kukosa huduma za matibabu mapema.
“Mtu mwenye ugonjwa wakifafa akichelewa kupata matibabu anaweza kupoteza maisha mapema kutoka na madhara mbalimbali ikiwemo kudondoka sehemu zenye hatari ikiwemo kwenye moto au kugongwa na gari” amesemea Prof. Nagu.
Pamoja na hayo amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kuongeza vituo vya kutolea huduma na kuweka dawa muhimu ili kupunguza uwezekano wa mtoto anayezaliwa kupata ugonjwa wa kifafa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TEA, Prof. William Matuja amesema kuwa ugonjwa wa kifafa unasababishwa na magonjwa yanayoshambulia ubongo hasa wakati mtoto anapozaliwa, mtoto kupata ugonjwa wa degedege unaojirudia, malaria kupanda kichwani au kula vyakula vyenye vijidudu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Mohamed Janabi amesema kwa sasa kuna mabadiliko katika matibabu hivyo ni vyema wataalam kwenda sambamba na mabadilko hayo, pia amewataka kutumia kongamano hilo kujadili na kubadilishana uzoefu hasa katika maswala ya tiba.