TUNAWEKA MAZINGIRA WEZESHI KUVUTIA MASOKO YA BIDHAA ZA TIBA NA DAWA;WAZIRI UMMY
Posted on: October 19th, 2023Na. WAF - Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya imejipanga kuweka mazingira wezeshi ili bidhaa za tiba na dawa zitakazozalishwa na viwanda nchini Tanzania ziuwe hapa nchini, Afrika Mashariki na nchi zote za ukanda wa SADC.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo Oktoba 19, 2023 wakati wa kikao cha kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi kilichofanyika katika kumbi za Bunge Jijini Dodoma kujadili kuhusu azimio la kuridhia Mkataba wa kuanzishwa kwa Taasisi ya Dawa ya Afrika (Treaty for the Establishment of the African Medicines Agency - AMA)
Waziri Ummy amesema Ili viwanda vya ndani vya dawa viweze kupata soko, kwa sasa wawekezaji wa viwanda vya dawa wanasubiri mkataba wa AMA upite ili kuwavutia zaidi na waweze kuuza kwa watu zaidi ya milioni 500 wa ukanda wa SADC.
“Bado tunajukumu la kuimarisha mifumo ya kusimamia usajili na udhibiti wa bidhaa tiba za dawa ili kuweza kufikia matokeo chanya katika uwekezaji wa viwanda vya bidhaa tiba za Dawa nchini”. Amesema Waziri Ummy
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu-Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe amesema nchi za Afrika zimeungana kupitia mkataba wa AMA ili kuweza kutengeneza wataalam ambao watasaidia nchi moja moja huku akiongeza kuwa wataalamu hao watapatikana kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Uwepo wa AMA utasaidia kuratibu na kusaidia nchi wanachama wa Umoja wa Afrika katika kuboresha uwezo wa kudhibiti ubora wa bidhaa tiba hususan katika maeneo ambayo ni changamoto kwa nchi nyingi barani Afrika.
Taasisi hii itaisaidia Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba (TMDA) kutatua changamoto mbalimbali katika udhibiti wa bidhaa tiba ikiwemo upungufu wa wataalamu, uwepo wa njia zisizo rasmi katika maeneo ya mipaka na vituo vya forodha visivyoruhusiwa kuingiza bidhaa tiba.