Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SIKU YA KONDOMU DUNIANI KUADHIMISHWA DODOMA

Posted on: February 12th, 2025

Na Waf Dodoma

Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini (NASHCoP), Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) na Shirika la Aids Healthcare Foundation (AHF) kwa pamoja wataadhimisha siku ya Kondomu Duniani kwa mara ya kwanza nchini tarehe 13 Februari, 2025.

Kaimu Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini (NASHCoP) Dkt. Zeye Nkomela amesema maadhimisho hayo yatafanyika mkoani Dodoma katika mkutano na waandishi wa habari na ofisi yake tarehe 12 Februari, 2025 Jijini Dodoma.

Dkt. Nkomela amesema katika kutekeleza azma ya Serikali ya kutokomeza janga la UKIMWI ifikapo mwaka 2030 kwa mwaka 2025, Wizara imeamua kujumuika na mataifa mengine Duniani ambayo yamekuwa yakiadhimisha siku ya Kondomu tangu mwaka 2009 kama sehemu ya dhamira ya kupambana na kuenea kwa maambukizi ya VVU na magonjwa ya ngono.

"Katika maadhimisho hayo shughuli mbalimbali zitafanyika ikiwemo kuwakumbusha watu juu ya umuhimu wa kujikinga na VVU na UKIMWI, magonjwa ya ngono na mimba zisizotarajiwa, utoaji wa elimu juu ya matumizi sahihi ya Kondomu na kuhamasisha upatikanaji wa kondomu kwa wananchi," amesema Dkt. Nkomela.

Pia Dkt. Nkomela amesema Serikali imeamua kuiweka siku hii kuwa maalum ya maadhimisho kwakuwa tafiti zinaonesha kupungua kwa matumizi ya kondomu katika mikoa mbalimbali, na hivyo kuongeza hatari ya maambukizi mapya ya VVU na magonjwa ya ngono kwa makundi mbalimbali.

"Bado kuna dhana potofu na unyanyapaa kuhusu matumizi ya kondomu na hivyo baadhi ya watu wamejikuta wanashiriki katika ngono isiyo salama," amesema Dkt. Nkomela.

Naye Meneja Mkazi wa Shirika la AHF Tanzania Bi. Haika Mtui ameishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa siku hiyo na kukubali kuadhimishwa kitaifa kwa lengo la kuikumbusha jamii jinsi gani matumizi ya kondomu yanaweza kupunguza maambukizi ya VVU, magonjwa ya ngono na mimba zisizotarajiwa.