SERIKALI YAONGEZA HUDUMA ZA KIBINGWA MIKOA YA NYANDA ZA JUU KUSINI
Posted on: May 6th, 2026Na Shaban Juma, Dodoma
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema huduma za kibingwa kwa magonjwa ikiwemo moyo, kansa, mapafu, figo na ini tayari zinatolewa katika Mikoa ya nyanda za juu kusini kupitia Hospitali za Rufaa na ya kanda.
Akijibu swali la Mbunge wa Iringa Mjini, Mhe. Fadhili Fabian Ngajiro, bungeni Dodoma Mei 6, 2026 kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, Dkt. Samizi amesema Serikali imeendelea kuimarisha huduma hizo ili kupunguza utegemezi wa rufaa kwenda mbali.
“Hospitali ya Kanda Mbeya inatoa pia huduma za ubingwa bobezi ikiwemo upasuaji wa moyo, upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu, matibabu ya mfumo wa chakula na ini, pamoja na huduma za mfumo wa upumuaji na upasuaji kwa watoto wachanga,” amesema.
Katika hatua nyingine, Dkt. Samizi amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa kituo maalum cha huduma za saratani mkoani Mbeya kitakachokuwa chini ya Taasisi ya Saratani Ocean Road.
Amesema kukamilika kwa kituo hicho, kinachojulikana kama ORCI Mbeya Cancer Centre, kutaongeza upatikanaji wa huduma za saratani katika kanda hiyo na kupunguza gharama kwa wananchi waliokuwa wakilazimika kusafiri hadi Dar es Salaam kufuata huduma hizo.