Wizara Ya Afya

SERIKALI YAIMARISHA UPATIKANAJI WA TAARIFA ZA MAABARA NCHINI

Posted on: June 11th, 2026

Na Cletus Sanga, WAF – Morogoro

Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la CIHEB Tanzania kupitia mradi wa Usalama wa Afya Duniani, inaendelea kuimarisha huduma za afya nchini kwa kuboresha mifumo ya upatikanaji wa taarifa za maabara, pamoja na kushirikiana na wadau katika kujadili na kutatua changamoto zilizopo katika eneo hilo.

Hayo yqmebainishwa na Mkuu wa Huduma za Maabara Mkuu wa Huduma za Maabara wa Wizara ya Afya, Bw. Reuben Mkala wakati wa kikao kazi cha kujadili na kuboresha upatikanaji wa taarifa za maabara kilichofanyika mkoani Morogoro.

Bw. Mkala amesema upatikanaji wa taarifa sahihi na kwa wakati ni nguzo muhimu katika kuboresha huduma za uchunguzi wa magonjwa, kwani taarifa hizo zinasaidia wataalamu wa afya kufanya maamuzi sahihi katika utoaji wa matibabu na udhibiti wa magonjwa.”

“Wizara ya afya itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha mifumo ya taarifa za maabara inaendelea kuimarishwa ili kuongeza ufanisi, ubora na upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi,” amesema Bw. Mkala.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mradi kutoka CIHEB Tanzania, Dkt. Edgar Lusaya amesema shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha mifumo ya afya nchini, hususan eneo la maabara na upatikanaji wa taarifa zinazosaidia katika utekelezaji wa programu mbalimbali za afya.

Amesema wataendelea kutoa ushirikiano wa kitaalamu na kiufundi katika juhudi za Serikali za kuboresha huduma za maabara na kuhakikisha taarifa zinazozalishwa zinatumika ipasavyo katika kuboresha afya ya wananchi.