SERIKALI YA USWIZI KUSHIRIKIANA NA TANZANIA KATIKA KUBORESHA SEKTA YA AFYA.
Posted on: April 15th, 2023Waziri wa Afya Mh Ummy Mwalimu, amekutana na balozi wa Uswizi nchini Tanzania na kuzungumza kuhusu mambo mbalimbali ikiwemo kushirikiana katika kuboresha Sekta ya Afya.
Akizungumza kwenye kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa NIMR jijini Dar es Salaam, Mh. Ummy Mwalimu ameishukuru Serikali ya Uswizi kupitia balozi wake Bw. Didier Chassot kwa ushirikiano wanaoutoa kwa wananchi wa Tanzania kuhusu mfuko wa pamoja (Basket fund).
Katika kikao hicho, Waziri Ummy ameyaangazia mambo manne yanayofanywa, ikiwemo mchango katika (HPSS), Uimarishaji wa huduma za Bima za jamii (CHF), udhibiti wa ugonjwa wa Malaria kupitia mradi mpya utakaowasilishwa na Wizarani na mwisho kabisa ni mchango kupitia huduma ya afya na kujengea uwezo vijana kushirikiana na Sekta nyingine nchini.
Katika hatua nyingine Mhe. Ummy ameiomba Serikali ya Uswizi kushirikiana na Tanzania katika kuboresha huduma za Afya kwa jamii kupitia CHW's.
Naye, balozi wa Uswizi nchini Bw. Didier Chassot ameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna inavyoweka juhudi kubwa kwenye usimamizi wa afya kwa wananchi, huku akitolea mfano namna ambavyo ugonjwa wa mlipuko wa Marburg ulivyodhibitiwa nchini.
Sambamba na hilo Bw. Chassot kupitia Serikali yake ameahidi kuendelea kutoa mchango katika uratibu wa pamoja baina ya Serikali yake, Serikali ya Tanzania na wadau wa Sekta ya afya kwa ujumla.
Kwa kuongezea Bw. Chassot ameahidi kushirikiana na Tanzania katika kuanzisha kituo cha umahiri cha utoaji wa huduma za kidigitali kwenye Sekta ya Afya nchini (Center for the Digital Health Technology) ili kuweza kurahisisha utoaji wa huduma za kiafya nchini.
Mwisho.