Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI, WADAU KUJA NA MIKAKATI YA PAMOJA KUKABILI MAGONJWA YASIYOPEWA KIPAUMBELE

Posted on: December 16th, 2025

Na WAF, Morogoro

Serikali kupitia Wizara ya Afya, chini ya Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa yasiyopewa kipaumbele, Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI, Wizara ya Elimu Sanyansi na Teknolojia pamoja na RUWASA kwa kushirikiana na Helen Keller International, pamoja wamekutana na kuja na afua za Maji, Usafi wa Mazingira na Magonjwa ayaliyokuwa hayapewi kipaumbele.

Akizungumza katika Jukwaa hilo la 7, Desemba 15, 2025, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Ubora wa Maji kutoka Wizara ya Maji Bw. Mteki Heri Chisute amesema kuwa, magonjwa hayo yamekuwa na athari kubwa kiafya, kijamii na kiuchumi, hivyo kuathiri uwezo wa wananchi kushiriki kwenye shughuli za maendeleo, huku muda mwingi ukitumika kujiuguza maradhi

“Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), yapo magonjwa 21 yaliyokuwa hayapewi kipaumbele duniani na kati ya hayo magonjwa 15 yanapatikana nchini mwetu, na kati ya hayo magonjwa matano (5) yapo kwenye mkakati wa kitaifa wa kuyatokomeza ikiwemo magonjwa yanayohusiana moja kwa moja na maji, na usafi wa mazingira kama vile Trakoma na Minyoo Tumbo” amesema Chisute

Aidha amesema kuwa serikali kwa kushirikiana na wadau imekuwa ikitekeleza afua za kudhibiti magonjwa hayo zikiwemo, umezeshaji wa kingatiba katika jamii na shuleni, uboreshaji wa upatikanaji wa maji safi na salama, Utoaji wa elimu ya afya na usafi wa mazingira, na huduma za matibabu kwa walioathrika.

Bw. Chisute amesisitiza kuwa serikali chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha mazingira wezeshi ya sekta ya Afya, Maji, Elimu, Fedha na Uratibu, ambapo msingi wa maboresho hayo ni uimarishaji wa ushirikiano wa kisekta, kuongeza uwajibikaji, na kushirikisha wadau wa karibu Zaidi ili kuunganisha nguvu katika mapambano dhidi ya magonjwa haya.

Katika hatua nyingine amelipongeza na kuwashukuru shirika la Helen Keller International kwa kuwezesha kufanyika kwa mkutano huu muhimu, na kuwaomba kuendelea kushirikiana na serikali katika kupambana na magonjwa haya kwa manufaa ya Watanzania.