Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI, WADAU KUENDELEZA AFUA KUKABILI KIPINDUPINDU

Posted on: December 19th, 2024

Na WAF – Dar es Salaam

Serikali na wadau wa maendeleo ya afya wameendelea kupambana na ugonjwa wa kipindupindu kwa kuchukua hatua madhubuti, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa usafi wa mazingira ili kuhakikisha hali ya upatikanaji wa maji safi na salama.

Hayo yamebainishwa Desemba 17, 2024, na Mkurugenzi wa Huduma za Kinga, Dkt. Ntuli Kapologwe, wakati wa zoezi la tathmini ya mwenendo wa ugonjwa wa kipindupindu nchini, lililowakutanisha Wakurugenzi wa Halmashauri, waganga wafawidhi, na wataalamu wa afya kutoka Wizara ya Afya.

Dkt. Ntuli amesema dhumuni kubwa la kikao kazi hicho ni kufanya tathmin ambayo itasaidia kuibua changamoto na kuziandalia mipango kazi kwa ajili ya kuboresha afua za kipindupindu

“Napenda kuwakumbusha viongozi juu ya jukumu letu la kuboresha afya za wananchi,” amesema Dkt. Ntuli.

Dkt. Ntuli amesisitiza kuwa, hatua muhimu ni kuhakikisha msaada wa haraka unapatikana kwenye maeneo yaliyoathirika na kipindupindu.

Aidha, Dkt. Ntuli amewataka waganga wafawidhi wa mikoa kufuatilia kwa karibu na kutathmini hatua zilizotekelezwa, ili kubaini maeneo yanayohitaji maboresho zaidi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wakurugenzi wa Halmashauri, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Wakili Kiomoni Kibamba, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Wakurugenzi wa Halmashauri na waganga wafawidhi.

“Ushirikiano huu ni muhimu katika kuhakikisha utekelezaji wa mikakati ya kudhibiti ugonjwa wa kipindupindu, kuboresha huduma za afya, na kuimarisha usafi wa mazingira katika maeneo yao,” Amesema wakili Kibamba.