SERIKALI MBIONI KUANZISHA KITUO MAALUM CHA KUHUDUMIA MAGONJWA YA MLIPUKO, KAGERA
Posted on: January 29th, 2025
Na WAF Kagera
Serikali ina mpango wa kujenga kituo maalum cha kuhudumia magonjwa ya mlipuko mkoani Kagera kitakachokuwa na vifaa vyote muhimu vya maabara ambavyo vitatumika kupima sampuli za vimelea vyote hatarishi sambamba na ujenzi wa kituo cha kutolea huduma za afya ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya.
Hayo yamebainishwa leo Januari 29, 2025 na Naibu Waziri wa Afya. Dkt. Godwin Mollel alipofika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Fatma Mwassa kumshukuru kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kudhibiti ugonjwa wa Marburg ulioikumba Wilaya ya Biharamulo mkoani humo ambao kwa sasa umedhibitiwa.
Dkt. Mollel amesema hatua hiyo ya Serikali inatokana na kutambua umuhimu wa kuwepo kwa kituo hicho mkoani humo kutokana na hali halisi kuwa mkoa unapakana na nchi jirani nne hivyo kuwa rahisi kupata magonjwa ya mlipuko kutokana na mwingiliano uliopo.
Akizungumzia ujenzi wa kituo cha kutolea huduma za afya amesema fedha zimeshatengwa kwa ajili ya ujenzi huo na mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa itajayopewa kipaumbele na kwamba kipaumbele cha sasa ni kuboresha huduma za afya katika ngazi ya msingi.
“Tunahitaji kufanya maboresho mengi mipakani ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa tunakuwa na watumishi ambao ni waadilifu wakati wote, amesema Dkt. Mollel.
Aidha Dkt. Mollel amesema Serikali pia itahakikisha kuwa kamati za ulinzi na Usalama za mkoa zinapatiwa mafunzo mbalimbali ya afya kwani wamekuwa wakitoa msaada mkubwa majanga yanapotokea.
Wakati huohuo ameiagiza Bohari Kuu ya Dawa kuhakikisha kuwa inawapatia wakuu wa mikoa na wilaya nakala ya taarifa za dawa ilizosambaza katika hospitali zilizopo katka eneo husika ili kuwa na ufuatiliaji wa karibu.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Fatma Mwassa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan Kwa hatua za haraka alizozichukua kwa kutoa fedha za kukabiliana na ugonjwa wa Marburg mkoani Kagera.