SERIKALI KUANZA UJENZI WA MAJENGO MAPYA HOSPITALI YA RUFAA TEMEKE MWAKA 2025/26
Posted on: May 14th, 2025
Na, WAF-Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya imebainisha kuwa ipo katika hatua za maandalizi ya usanifu wa jengo jipya la Huduma za Kliniki za Kibingwa na Bima katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke, Dar es Salaam. Ujenzi wa jengo hilo unatarajiwa kuanza rasmi katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Akijibu swali la Mbunge wa Temeke, Mhe. Dorothy George Kilave, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema hatua hiyo ni sehemu ya maboresho ya miundombinu ya Hospitali za Rufaa za mikoa nchini kote.
Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Liwale Mhe. Zuberi Kuchauka ametaka kufahamu mkakati wa serikali katika kuongeza madaktari bingwa katika hospitali hiyo, akibainisha kuwa bado kuna upungufu mkubwa wa wataalamu hao. Dkt. Mollel amejibu kuwa serikali itaendelea kupeleka madaktari bingwa kadri ya uhitaji, licha ya kwamba Hospitali ya Temeke tayari ina madaktari bingwa wengi ukilinganisha na maeneo mengine.
Aidha, kuhusu Hospitali ya Mkoa wa Lindi, Dkt. Mollel ameeleza kuwa serikali inaendelea na upembuzi yakinifu pamoja na michoro ya usanifu kwa lengo la kuiboresha hospitali hiyo ili ifikie viwango vya hospitali nyingine za mikoa.
Kwa upande mwingine, Mbunge wa viti maalum Mhe. Aysharose Mattembe amehoji kuhusu ucheleweshaji wa ukamilishaji wa Hospitali ya Mkoa wa Singida. Dkt. Mollel amehakikishia Bunge kuwa ujenzi wa hospitali hiyo utakamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu, Desemba 2025, kwani vikwazo vyote vilivyokuwa vikichelewesha mradi huo vimeshatatuliwa.