Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

RC BABU AWATAKA WANAKILIMANJARO KUCHANGAMKIA KAMBI YA MADAKTARI BINGWA

Posted on: December 5th, 2024

Na WAF, MOSHI

Wananchi mkoani Kilimanjaro wametakiwa kuchangamkia huduma za Kibingwa na Ubingwa Bobezi unaotolewa kwa siku tano kwa Kanda ya Kaskazini

Kauli hiyo ya Mkuu wa mkoa ameitoa leo Desemba 04, 2024 ikiwa ni Siku tatu baada ya kuanza kwa kambi hiyo iliyosheheni Madakatari Bingwa kutoka Mikoa yote ya Kanda ya Kaskazini shabaha ikiwa ni kushusha huduma hizo za Kibingwa.

Mhe. Babu amesema, wananchi wa mkoa huo na mikoa jirani wanayo kila sababu ya kumshukuru Rais Samia kwa Ubunifu huo wa kuwashusha Madaktari Bingwa hadi ngazi chini kwa wingi wao.

"Mtakumbuka siku chache zilizopita tulikuwa na kambi ya kibingwa kwa wilaya zote, lakini leo Mhe. Rais ametuletea Mabingwa na Bobezi ambao kwa wingi wao wameweka kambi katika Hospitali yetu ya Mawenzi lengo likiwa kuhudumia wananchi wa Kanda yote ya Kaskazini huu ni upendo wa pekee," amesema Mhe. Babu.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya ufunguzi, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa Mawenzi Dkt Edna-Joy Munisi amesema , wananchi zaidi ya 1300 wamepata huduma hiyo ya Madaktari Bingwa na kuongeza kuwa wagonjwa 22 wamefanyiwa upasuaji mdogo na mkubwa kwenye kambi hiyo inayoendelea mkoani hapo.