NAKALA YA FOMU YA DAWA NI HAKI YA WAGONJWA, WASINYIMWE
Posted on: February 18th, 2025
Na WAF, Tosamaganga - Iringa
Kaimu Mkurugenzi Huduma za Tiba ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Kinywa na Meno Dkt. Baraka Nzobo amezitaka hospitali zote nchini kutambua kwamba ni haki ya mgonjwa kupatiwa nakala ya Fomu ya Dawa mara baada ya kutibiwa ili itakapotokea changamoto yoyote aweze kusaidiwa na kupatiwa huduma sahihi kulingana na dawa alizotumia awali.
Dkt. Nzobo ameyasema hayo Februari 13, 2025 wakati wa zoezi la usimamizi shirikishi linaoloendelea mkoani Iringa katika Hospitali ya Halmashauri ya Iringa, Hospitali ya Mji Mafinga na Hospitali Rufaa ya Mkoa ya Tosamaganga, mkoani hapo.
Dkt. Nzobo amesema mara baada ya mgonjwa kuandikiwa na kupatiwa dawa anatakiwa apate nakala ya fomu za dawa alizopatiwa kwakuwa cheti ni haki yake na haitakiwi kunyimwa ili kisaidie kutengeneza mnyororo wa mfumo wa matibabu ya mgonjwa.
“Nitoe wito kwa hospitali zote nchini, kuwapatia wagonjwa nakala za cheti cha dawa kwani nakala hizo zinamlinda mgonjwa, na faida ya hili ni inapotokea mgonjwa amepata changamoto ya dawa au madhara yoyote inakuwa rahisi kuonesha cheti kama hadidu ya rejea,” amesema Dkt. Nzobo.
Ameongeza kuwa hilo limekuja baada ya kuona likijitokeza mara kadhaa katika baadhi ya maeneo ambayo wataalam wa Wizara ya Afya, OR-TAMISEMI na viongozi wa Afya ngazi za mikoa na wilaya wamekuwa wakiendesha zoezi la usimamizi shirikishi.
Kwa upande mwingine Dkt. Nzobo amesema changamoto zingine ambazo wameziona wamekuwa wakizitatua pamoja na watumishi wa kada ya afya waliopo vituoni.
“Wizara ya Afya ipo kwa ajili ya kila mtu, vituo vyote, vya Serikali, binafsi na Mashirika ya kidini, Wizara ya Afya itavihudumia na kuvisimamia kwa kutoa miongozo ili huduma bora ziendelee kutolewa kwa kila mtanzania,” amesema Dkt. Nzobo.
Wizara ya Afya imetumia Fursa hiyo pia kugawa vitabu vya mwongozo wa matibabu ya selimundo kwa watoa huduma, zoezi linaloendeshwa na Dkt. Asteria Mpoto na mpaka sasa zaidi ya vitabu 100 vimegawiwa kwenye Halmashauri 54 kutoka mikoa nane (8).