Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MSD SIMAMIENI UENDESHAJI WA VIWANDA VYA NDANI VYA BIDHAA ZA AFYA- MHAGAMA

Posted on: February 19th, 2025


Na WAF - Dar es Salaam

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama ameitaka Bohari ya Dawa nchini (MSD) kusimamia viwanda vya ndani vinavyozalisha bidhaa za afya ikiwemo dawa, maji dawa (drip) ili kuviwezesha viwanda hivyo kuendelea kukua na kusaidia katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Waziri Mhagama amesema hayo Februali 18, 2025 baada ya kutembelea viwanda vinavyozalisha bidhaa za afya ikiwemo kiwanda cha Pharmaceutical, Medical Devices, Medical Equipment Assembly, Raw materials (API), Common Utilities pamoja na Logistic Centre (Warehousing) vilivyopo Zegereni, kibaha mkoani Pwani.

Waziri Mhagama amesema, pamoja na kujenga historia ya Taifa hili, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezielekeza sekta binafsi kuhakikisha zinachangia katika ujenzi wa uchumi, ustawi wa wananchi na maendeleo endelevu ya Taifa la Tanzania.

"Hata sisi leo, tumekuja kuona wenzetu wa Sekta binafsi ni namna gani wanaweza kutumika kwenye maendeleo na hasa upande wa sekta ya afya, lakini tunajua kuna uwekezaji mkubwa mkoa wa Pwani ambao una zaidi ya viwanda 100 vilivyojengwa ndani ya muda mfupi," amesema Waziri Mhagama.

Amesema, Sekta ya Afya inauhitaji mkubwa wa uwekezaji wa viwanda nchini kwakuwa kwenye bara la Afrika zaidi ya asilimia 70-80 bidhaa za afya zinatoka nje ya nchi ingawa kuna changamoto ya ucheleweshaji wa bidhaa za afya kutoka nje, hivyo kuna manufaa bidhaa za afya zinapozalishwa nchini, ikiwemo kupunguza gharama kubwa ya bajeti ya nchi.

Amesema, faida nyingine za uzalishaji wa bidhaa hizo nchini ni pamoja na kupunguza utegemezi, kuwa na uhakika wa upatikanaji wa bidhaa hizo kwa kuzingatia mahitaji na matumizi ya nchi, kuchagua ni bidhaa gani ambazo zinahitajika zaidi pamoja na kuhifadhi fedha za kigeni ili zitumike kwenye uwekezaji wa maeneo mengine.

Aidha, Waziri Mhagama amesema kuwa Serikali inaanza kujipanga kuanza mkakati wa kuuza bidhaa za afya nje ya nchi kwakuwa tayari Serikali ya Tanzania imepata masoko ya kuuza bidhaa hizo nje ya nchi.