Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MIKOA 16 NCHINI YAWEZESHWA VITUO VYA KURATIBU DHARURA ZA KIAFYA, MAJANGA

Posted on: November 12th, 2024

Na-WAF Manyara

Serikali kupitia Wizara ya Afya imesema hadi sasa mikoa 16 imewezeshwa kuanzisha na kuendesha vituo vya kuratibu dharura za kiafya na majanga (EOC), Manyara ukiwa mkoa wa 17 ikiwa ni mikakati ya Serikali kujiimarisha katika kukabiliana na dharura zinazoweza kujitokeza.

Hayo yamebainishwa leo Novemba 12, 2024 mkoani Manyara na Dkt. Agnes Buchwa kwa niaba ya Mkurugenzi wa Huduma za Dharura na Maafa Wizara ya Afya, Dkt. Elias Kwesi wakati akifungua mafunzo ya jinsi ya kukabiliana na dharura za kiafya na majanga kwa Timu ya Uendeshaji wa Huduma za Afya ya Mkoa wa Manyara (RHMT), wataalam wa sekta ya mifugo, Maji, kilimo na habari.

“Mafunzo haya yatawasaidia wataalamu mliohudhuria leo kuongeza ujuzi na weledi wa kuratibu, kujiandaa, kudhibiti na kukabiliana na matukio ya dharura za kiafya na majanga kwa kutumia kituo cha kuratibu dharura za kiafya na majanga ambacho kimeanzishwa katika mkoa wenu ambacho kipo katika hatua za mwisho kukamilika na kuanza kutumika,” ameeleza Dkt. Buchwa.

Dkt. Buchwa amesma kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo katika kuratibu, kujiandaa kudhibiti na kukabiliana na dharura zote za kiafya na majanga yanayoweza kuleta madhara kwa binadamu, wanyama na mazingira.

Dkt.Buchwa amesema Mkoa wa Manyara kama ilivyo mikoa mingine imekuwa ikikabiliana na matukio mengi ya dharura yanayoleta madhara si tu kwa binadamu lakini pia kwa wanyama na mazingira, hivyo mafunzo hayo yatasaidia kuimarisha huduma zote za dharura.

Hata hivyo Dkt. Buchwa amekumbushia tukio la Disemba 2023 la maporomoko ya udongo wilayani Hanang, mlipuko wa ugonjwa wa mazao wa sumu kuvu ambao umekuwa ukijitokeza mara kwa mara, mafuriko na ukame kwa baadhi ya wilaya, yanahitaji uratibu na ushiriki wa pamoja wa wataalamu na rasilimali nyingine kutoka taasisi mbalimbali nje ya sekta ya afya pamoja na wananchi.

Aidha mafunzo hayo yatatolewa kwa muda wa siku tano (5) na kuratibiwa na Wataalamu kutoka katika kituo cha kuratibu dharura za kiafya na majanga (ECO) cha Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani, ofisi ya Tanzania.