Wizara Ya Afya

MAGEUZI NHIF KUONGEZA UFANISI WA HUDUMA

Posted on: October 22nd, 2026

Na Andrea Kadege, WAF-Mtwara


Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa, amesema Serikali inaendelea kufanya mageuzi katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa lengo la kuongeza ufanisi, kupanua wigo wa huduma na kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Awamu ya Pili ya Bima ya Afya kwa Wote uliofanyika katika viwanja vya Sabasaba mkoani Mtwara, Oktoba 22, 2026, Mhe. Mchengerwa amesema mageuzi hayo yanalenga kuifanya NHIF iweze kuhudumia idadi kubwa zaidi ya Watanzania kwa kuzingatia mahitaji ya mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote.


"Serikali inalenga kuboresha matumizi ya mifumo ya kidijitali katika usajili wa wanachama, uhakiki wa taarifa na malipo, hatua itakayosaidia kuongeza uwazi na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wanachama na vituo vya kutolea huduma za afya" amesema Mchengerwa


Aidha amesisitiza umuhimu wa madai ya vituo vya afya kulipwa kwa wakati, pamoja na kulinda michango ya wanachama dhidi ya matumizi yasiyo sahihi na vitendo vya udanganyifu vinavyoweza kuathiri uendelevu wa mifumo ya bima.


Amefafanua kuwa mageuzi hayo yanaenda sambamba na juhudi za Serikali za kuboresha ubora wa huduma za afya na kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi husika ili kuhakikisha Bima ya Afya kwa Wote inatekelezwa kwa ufanisi na kuwanufaisha wananchi.


Amesema Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa mageuzi hayo kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya afya ili kuhakikisha mifumo ya bima inakuwa imara, endelevu na yenye uwezo wa kutoa huduma bora kwa wananchi.