Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MADAKTARI BINGWA WA SAMIA WAFANIKISHA UPASUAJI KUONDOA UVIMBE TUMBONI KWA MAMA WA MIAKA 50

Posted on: September 20th, 2025

Na WAF - Ileje Songwe

Madaktari Bingwa wa magonjwa ya uzazi wa kambi ya Madaktari Bingwa wa Mama Samia mkoani Songwe imefanikiwa kutoa huduma ya upasuaji kwa mwanamke mwenye umri wa miaka 50 aliyekuwa anasumbuliwa na maumivu makali ya tumbo yaliyosababishwa na uvimbe.

Mama huyo alifikishwa katika Hospitali ya wilaya ya Ileje iliyopo Itumba akitokea kijiji cha Mlale akisumbuliwa na tatizo hilo kwa muda mrefu ya zaidi ya miaka mitatu.

Akizungumza baada ya upasuaji huo Dkt. Sister Mpeli Mwakyelu amesema baada ya uchunguzi wa kina na vipimo mbalimbali, madaktari waligundua kuwa ana uvimbe tumboni wa aina ya fibroid, pamoja na upungufu wa damu uliosababisha hali yake kuwa mbaya.

Kwa kuzingatia hali yake, timu ya madaktari ilianza kwa kumtibu kwa kumpatia damu chupa mbili ili kuimarisha afya yake kabla ya kufanyika kwa upasuaji wa kuondoa uvimbe huo.

“Tumefanikisha upasuaji wa kuondoa uvimbe unaokadiriwa kuwa na kilo 5, ambao ulikuwa unamletea maumivu makali na changamoto za kiafya. Upasuaji umefanikiwa kwa mafanikio makubwa, na mama anaendelea vizuri kwa uangalizi wa karibu wa madaktari wetu,” - amesema Dkt. Sister Mwakyelu.

Dkt. Sister Mwakyelu amehimiza jamii kuchukua tahadhari na kujitokeza kwa wakati ili kupata huduma za afya zinazostahili, pamoja na kujua afya zao na kufanya uchunguzi wa mara kwa mara ili kuzuia matatizo makubwa ya kiafya.