Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MADAKTARI BINGWA 49 WA RAIS SAMIA WATIA KAMBI MOROGORO.

Posted on: October 15th, 2024

Na WAF - Morogoro

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima amewapokea Madaktari Bingwa 49 wa Rais Samia kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu kwa siku sita katika hospitali za halmashauri za mkoa huo.

Mapokezi hayo yamefanyika Oktoba 14, 2024 katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro.

Mhe. Malima amesema wananchi wa mkoa huo wanauhitaji wa huduma za matibabu ya kibingwa, hivyo uwepo wa kambi hiyo ni mkombozi kwa wananchi hao katika kutatua changamoto zao za kiafya.

“Nimshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuwasambaza madaktari bingwa hawa katika hospitali zetu za halmashauri lakini pia nimshukuru Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama kwa kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais, kazi mnayokwenda kuifanya madaktari bingwa kwa kuwahudumia wananchi ni kazi kubwa mno mjue sisi wana Morogoro tunawahitaji, tunawathamini na tunawapenda,” amesema Mhe. Malima.

Aidha Mhe. Malima ameeleza kuwa uwepo wa Madaktari Bingwa wa Rais Samia katika hospitali za halmashauri sio jambo la kisiasa ni jambo kubwa la kuokoa maisha na kuboresha Afya za wananchi.

Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa ameahidi ushirikiano kwa kipindi chote Madaktari Bingwa hao watakapokuwa mkoani hapo wakiwahudumia wananchi na kutoa rai kwa wananchi kujitokeza kwa wingi ili kupata huduma hizo za kibingwa zilizosogezwa karibu na maeneo yao.

Akitoa salamu za Wizara ya Afya Mratibu wa Kambi mkoa wa Morogoro Dkt. Ismail Mohammed Mtitu amesema lengo kubwa la kupeleka Madaktari Bingwa wa Rais Samia ni kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi ili kupunguza gharama za matibabu na kuondoa rufaa , kuanzisha wodi za kuhudumia watoto wachanga pamoja na kutoa mafunzo elekezi kwa wataalam waliopo katika hospitali za halmashauri.