MAABARA YA KIBONG'OTO KUFIKIA NGAZI YA NNE;MHE.UMMY
Posted on: July 15th, 2022Na. Catherine Sungura, Siha
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amemuahidi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Phillip Mpango kuwa Maabara ya afya ya jamii ya Kibong'oto baada ya muda itafika ngazi ya 4 itakayoweza kutengeneza chanjo ya magonjwa mbalimbali.
Waziri Ummy amesema hayo leo wakati wa uzinduzi wa Maabara hiyo iliyopo katika Hospitali ya Kibong'oto Wilayani Siha inayotegemewa kupima sampuli ya magonjwa mbalimbali ambukizi .
"Hapa nchini kwa sasa zipo maabara mbili za namna hii ambayo ni hiyo ya Kibong'oto na ile ya Dar es Salaam. Napenda kuwatoa hofu watanzania kwamba hivi sasa nchi ina uwezo wa vifaa na wataalam wa kupima sampuli za magonjwa magonjwa mbalimbali ambukizi". Amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy ameongeza kuwa Maabara hiyo haitajikita tu kwenye TB bali magonjwa menginevya kuambukiza kama Chikungunya, Murbug, UVIKO-19 na mengineyo.
Waziri Ummy amesema hivi sasa wagonjwa wa TB wamepungua ambapo mwaka 2015 kati ya watu 100,000 kulikua na wagonjwa 306 na mwaka 2021 kati ya watu 100,000 kulikua na wagonjwa 222 sawa na upungufu wa 54%.
Kuhusu vifo vitokanavyo na TB Waziri Ummy amesema Mwaka 2015 kulikua na vifo 56,000 kati ya watu 100,000 ambapo mwaka 2021 kulikua na vifo 26,800 kati ya watu 100,000 sawa na upungufu wa 52%.