Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

KANADA YATOA SHILINGI BILIONI 240 KWENYE MFUKO WA AFYA WA PAMOJA

Posted on: July 20th, 2023

Na. WAF Dodoma


Serikali ya Kanada imetoa kiasi cha Shilingi Bilioni 240 kwenye Mfuko wa Afya ya pamoja (Health Basket Fund) ili kusaidia Sekta ya Afya nchini.


Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amebainisha hayo leo Julai 20, wakati wa mkutano wa utekelezaji wa shughuli za Mfuko wa Afya wa Pamoja (Health Busket Fund) HBF na Waziri wa Maendeleo ya jamii Kanada Jijini Dodoma.


“Tunaishuku sana Serikali ya Kanada kupitia Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Kanada Mhe. Harjit Sajjan kwa kusaidia  Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kiasi cha shilingi Bilioni 240 kwa ajili ya kuboresha sekta ya afya”, akishukuru Waziri Ummy


Aidha, Waziri Ummy ameeleza kuwa kati ya kiasi hicho shilingi Bilioni 140 zinaingia serikalini kwa ajili ya kuchangia mfuko wa afya wa pamoja ambapo mpaka sasa Serikali ishapokea kiasi cha shilingi Bilioni 94 ambazo zimeelekezwa kwenye akaunti za ngazi ya msingi ambazo ni zahanati na vituo vya afya nchini.


Amesema, Vituo vya afya na Zahanati watapanga vipaumbele vyao ikiwemo kununua dawa, uzazi salama, kulipia umeme, kulipia maji na wanatumia kufanya ukarabati mdogo pamoja na kununua vifaa tiba.


“Kwa ujumla mchango wa Serikali ya Kanada kwa Tanzania umeleta matokeo mazuri kwa Huduma za afya Tanzania leo tunaongea wanawake karibu asilimia 90 wajawazito wanajifungulia katika vituo vya kutoa Huduma za afya kwa sababu ya mchango wa Kanada”, amesema Waziri Ummy.


Pia ameongeza kuwa wamepunguza vifo vya watoto wachanga na wenye umri chini ya miaka mitano kutoka vifo 67 katika kila vizazi hai 1000 hadi vifo 43. 


“Lakini pia tumeweza kupunguza mimba za utotoni kutoka asilimia 27 hadi asilimia 22, tumepunguza udumavu kutoka asilimia 38 na sasa tunazungumzia asilimia 31 na kwa watoto wetu wanapata chanjo”, Amesema Waziri Ummy.


Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Kanada Mhe. Harjit Sajjan amesema kuwa wametangaza miradi mitano mipya ya Afya yenye thamani ya dola za Kanada Milioni 128.5 ambapo dola za Kanada Milioni 75 kwa mfuko wa ruzuku wa shughuli za Mfuko wa Afya wa Pamoja (Health Sector Busket Fund, HSBF) kwa Serikali ya Tanzania na nyongeza ya dola za Kanada 500,000  kwa UNICEF kwa usaidizi wa kitaalam.


"Leo nina furaha pia kutangaza dola za Kanada milioni 23 katika ufadhili wa shirika la CanGIVE kwa miradi miwili mipya kwa ushirikiano na UNICEF Tanzania na shirika la Afya Duniani, Tanzania miradi hii ya CanGive itasaidia juhudi za watanzania kuchanja makundi yaliyopewa kipaumbele kwa njia ambayo itaimarisha huduma za afya kwa mapana zaidi”, Amesema Mhe. Sajjan