CHANGAMOTO ZIFANYENI KUWA FURSA KATIKA HUDUMA ZA AFYA ZA UBINGWA, UBINGWA BOBEZI
Posted on: February 19th, 2025
Na WAF - Dar es Salaam
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama ameitaka bodi mpya ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani, Tumbi kuongeza ubunifu katika utolewaji wa huduma bora za afya ikiwemo huduma za ubingwa na ubingwa bobezi pamoja na kuzifanya changamoto zilizopo kuwa fursa katika hospitali hiyo.
Waziri Mhagama ametoa maelekezo hayo leo Februari 18, 2025 Mkoani Pwani baada ya kuzindua bodi hiyo mpya ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Pwani, Tumbi inayosimamiwa na kuongozwa na Mwenyekiti wake Bi. Zalia Kawawa Mbeo yenye wajumbe tisa(9).
“Hakikisheni mnafuatilia masuala yote yanayohusu hospitali yetu ya Rufaa ya Tumbi pamoja na kulinda uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambao ni zaidi ya Shilingi Trilioni 6.7 zimewekezwa katika Sekta ya Afya, pamoja na kununua magari ya wagonjwa na kuyaleta hapa ili iwasaidie kukamilisha mipango yenu vizuri,” amesema Waziri Mhagama.
Pia, Waziri Mhagama ameitaka Bodi hiyo kulinda na kusimamia rasilimali watu ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za kukutana na watumishi wa hospitali hiyo kwa kuzungumza nao ili kama wanachamgamoto waweze kuzigeuza kuwa fursa kwao.
“Agizo langu jingine kwa bodi, simamieni vizuri rasilimali watu ni rasilimali muhimu kwakuwa kama huna watu wa kufanya kazi huwezi kufanikiwa, ukiwa na fedha kama huna rasilimali watu wanaoweza kusimamia fedha huwezi kufanikiwa,” amesema Waziri Mhagama.
Aidha, Waziri Mhagama amesema Sera ya Afya ya mwaka 2007, kipengere cha 8.2 imeelekeza kuwepo kwa vyombo vya kisheria, ikiwa ni pamoja na uwepo wa bodi katika hospitali zote za Rufaa za Mikoa na zitateuliwa bodi hizo na mamlaka husika.
“Kwa hiyo ninawakumbusha bodi kuwa mpo hapa kisheria na mnafanya kazi kisheria, msiogope, tekelezini majukumi yenu kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo, lakini msitishe watu kwa kukiuka sheria na taratibu zilizopo,” amesema Waziri Mhagama.