BMH YAVUNA FIGO BILA UPASUAJI KWA MARA YA KWANZA
Posted on: November 14th, 2024
Na WAF, Dodoma
Wataalamu wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa kushirikiana na Wataalamu kutoka Shirika la ZGT Overzee la Uholanzi, wamefanikiwa kuvuna figo kwa mtu (jina limehifadhiwa) bila kufanya upasuaji, zoezi linalojulikana kitaalamu kama Laparoscopic Nephrectomy ili kwenda kuipandikiza kwa mgonjwa wa figo.
Hii ni mara ya kwanza kwa BMH kuvuna figo pasipo upasuaji kutoka kwa mtu ambaye anamchangia figo ndugu yake mwenye matatizo ya figo tangu BMH ilipoanzisha huduma ya upandikizaji figo miaka sita iliyopita.
BMH ilikuwa ni Hospitali ya pili ya Umma kuanzisha huduma ya upandikizaji figo mwaka 2018. Aina hiyo ya matibabu ya Laparoscopic Nephrectomy imefanyika leo hospitalini hapo kwenye kambi maalum ya matibabu ya Madaktari Bingwa wa BMH wanaoshirikiana na Madaktari Bingwa kutoka Uholanzi, ambao watakuwepo hadi Novemba16, 2024.
Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Prof. Abel Makubi, amesema kuwa huduma hiyo haihusishi kumfanyia upasuaji mtu anaemchangia figo mgonjwa wa figo, badala yake figo inatolewa kupitia kitundu kidogo.
Ametaja faida ya huduma hiyo kuwa ni kuondoa changamoto ya mgonjwa kuugua muda mrefu au kulazwa kwa muda mrefu kwa kuwa kidonda kinapona mapema.
“Faida nyingine ni kupunguza gharama za dawa nyingi kutumika kwa mgonjwa wakati amelazwa,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa BMH.