Wizara Ya Afya

WIZARA YA AFYA YAIMARISHA UTAAYARI WA WATUMISHI KUKABILIANA NA EBOLA SERENGETI

Posted on: September 1st, 2026

Na Happyness Hans, WAF - Mara

Wizara ya Afya kupitia idara ya dharura na maafa, kitengo cha uhakiki ubora kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI pamoja na Shirika la afya Duniani (WHO) imetoa mafunzo kwa watumishi wa afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kujikinga na kukabiliana na ugonjwa wa Ebola pamoja na magonjwa mengine ya milipuko, huku wakihakikisha wanatoa huduma salama kwa wagonjwa.

Amesema hayo leo Septemba 1, 2026, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Michael Kiremeji, wakati timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Afya na WHO walipotembelea Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kwa ajili ya kutoa mafunzo na kutathmini utayari wa watumishi wa afya katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko.

Dkt. Kiremeji amesema Serengeti ni miongoni mwa maeneo yanayohitaji maandalizi ya kutosha kutokana na kuwa karibu na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ambayo hupokea watalii kutoka mataifa mbalimbali. Amesema hali hiyo inaongeza umuhimu wa kuhakikisha watumishi wa afya wanakuwa tayari kujilinda na kuwahudumia wagonjwa endapo magonjwa ya milipuko yataingia katika eneo hilo.

Kwa upande wake, Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Serengeti amesema wamepokea wataalamu hao kutoka Wizara ya Afya kwa ajili ya kuangalia maandalizi na utayari wa hospitali katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko, hususan Ebola. Amesema wataalamu hao wameangalia hatua mbalimbali kuanzia kumpokea mgonjwa anayeshukiwa hadi kumfikisha katika eneo maalum la matibabu.

Amesema ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwa hospitali hiyo, kwani wataalamu wamezunguka maeneo mbalimbali na kubaini baadhi ya mapungufu yanayohitaji kuboreshwa. Ameongeza kuwa wamefundishwa mambo mbalimbali kuhusu namna ya kujiandaa na milipuko na wamekumbushwa taratibu muhimu za kuzingatia, huku akiahidi kuwa maelekezo yote yaliyotolewa yatafanyiwa kazi.

Nao watumishi wa afya wa Kituo cha Afya Mugumu wamesema mafunzo hayo yamewapatia maarifa na ujuzi utakaowawezesha kutoa huduma bora na salama kwa wagonjwa wa magonjwa ya milipuko.