Wizara Ya Afya

WIZARA YA AFYA YAANDAA MWONGOZO WA KUKABILIANA NA UGONJWA WA EBOLA NA MARBURG

Posted on: October 1st, 2026

Na Happyness Hans, WAF - Morogoro

Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) imehuisha mwongozo wa matibabu, kinga na udhibiti wa maambukizi ya magonjwa ya milipuko, hususan Ebola na Marburg, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha maandalizi ya nchi kukabiliana na magonjwa hayo endapo yatajitokeza. Mwongozo huo unalenga kuwawezesha wataalamu wa afya kutoa huduma kwa kuzingatia taratibu na viwango vinavyokubalika, sambamba na kuhakikisha usalama wa watoa huduma.

Akizungumza leo oktoba 1,2026 kuhusu hatua hiyo, Afisa wa Uimarishaji Ubora, Kinga na Udhibiti wa Maambukizi kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Radenta Bahegwa, amesema mwongozo huo umeainisha njia na viwango mbalimbali vinavyopaswa kuzingatiwa na wataalamu wa afya wakati wa kutoa huduma kwa wagonjwa wa Ebola na Marburg.

Dkt. Radenta amesema hadi sasa hakuna kisa cha Ebola au Marburg kilichothibitishwa nchini, akieleza kuwa maandalizi hayo yanafanyika kwa lengo la kuhakikisha wataalamu wa afya wanakuwa tayari kutoa huduma endapo magonjwa hayo yatajitokeza.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mpango wa Kinga na Udhibiti wa Maambukizi (IPC), Dkt. Joseph Hokororo, amesema kikao hicho kinalenga kuhuisha mwongozo wa matibabu, kinga na udhibiti wa magonjwa ya milipuko ili uendane na miongozo ya kimataifa iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO), Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa vya Marekani (CDC) pamoja na CDC Afrika.

Amesema kuwa uwepo wa mwongozo huo ni sehemu ya maandalizi ya nchi kuhakikisha inakuwa tayari wakati wowote anapojitokeza mgonjwa au mtu anayeshukiwa kuwa na Ebola au Marburg. Aidha, mwongozo huo unalenga kuhakikisha watoa huduma wanazingatia hatua stahiki za kinga na usalama wakati wa kutoa huduma kwa wagonjwa wa magonjwa ya kawaida na magonjwa ya milipuko yanayoambukiza.

Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Wizara ya Afya katika kuimarisha mifumo ya maandalizi na mwitikio dhidi ya magonjwa ya milipuko, kwa kuhakikisha wataalamu wa afya wanakuwa na maarifa, miongozo na taratibu zinazowawezesha kutoa huduma kwa usalama na ufanisi wakati wowote inapohitajika.