Wizara Ya Afya

PROF. SUNGUYA: TUSHIRIKIANE KUTEKELEZA VIPAUMBELE VYA WIZARA YA AFYA

Posted on: October 1st, 2026

Na Aisha Swahibu, WAF - Dodoma

Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Bruno Sunguya, amesema anaamini katika utendaji kazi unaozingatia ushirikiano na nguvu ya pamoja, ili kuhakikisha vipaumbele vya Wizara ya Afya vinatekelezwa na kufikiwa kwa ufanisi.

Prof. Sunguya ameyasema hayo leo, Oktoba 1, 2026, wakati wa mapokezi yake rasmi katika Ofisi za Wizara ya Afya, Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, ambapo alipokelewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, pamoja na viongozi na watumishi wa Wizara hiyo.

Amesema milango ya ofisi yake iko wazi kwa watumishi wote, akisisitiza kuwa hatokuwa kikwazo katika utekelezaji wa majukumu na mipango inayolenga kuimarisha huduma za afya nchini.

Aidha, Prof. Sunguya amesema yuko tayari kuendelea kujifunza kutoka kwa kila mmoja katika sekta ya afya, akieleza kuwa ushirikiano huo utasaidia kufikia lengo la pamoja la kuwatumikia wananchi na kuwapatia huduma bora za afya.

Amesema maendeleo ya sekta ya afya yanahitaji kila mmoja kutambua nafasi yake na kutekeleza wajibu wake kwa kushirikiana na wengine. Amesisitiza kuwa changamoto zilizopo hazipaswi kuwa kikwazo cha kufanya kazi kwa ufanisi na kufikia malengo yaliyowekwa.

Vilevile, Prof. Sunguya amesisitiza umuhimu wa kuwashirikisha watumishi katika maamuzi yanayohusu utekelezaji wa majukumu yao, akieleza kuwa ushirikishwaji hujenga uwajibikaji, umiliki wa maamuzi na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa mipango ya sekta ya afya.