KINGA YAHIMIZWA KUPEWA KIPAUMBELE KATIKA AFYA YA KINYWA NA MENO
Posted on: October 3rd, 2026Na Andrea Kadege, WAF–Dar es Salaam
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayeshughulikia Dawa na Vifaa Tiba, Bw. Emmanuel Tayari, amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika kinga, uchunguzi wa mapema na matibabu ya wakati katika kukabiliana na changamoto za afya ya kinywa na meno nchini.
Akizungumza leo Oktoba 2, 2026, wakati wa uzinduzi rasmi wa Kituo cha huduma za meno na vipandikizi cha Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam, Daud amesema afya ya kinywa ni sehemu muhimu ya afya ya mtu kwa ujumla, ikihusisha lishe, mawasiliano, kujiamini, uzalishaji na ubora wa maisha.
“Pale inapowezekana, tunapaswa kuweka mkazo katika kinga, utambuzi wa mapema na matibabu kwa wakati, badala ya kusubiri hadi hatua ya kung’oa jino iwe ya lazima,” amesema Bw. Tayari.
Amesema Serikali inaendelea kuimarisha huduma za afya ya kinywa nchini, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Afya ya Kinywa wa mwaka 2026–2031 unaolenga kuongeza upatikanaji wa huduma zenye usawa, nafuu na zinazomlenga mgonjwa.
Bw. Tayari amesema takwimu za National Oral Health Survey ya mwaka 2020 zinaonesha kuwa asilimia 76.5 ya watu wazima Tanzania wanaathiriwa na kuoza kwa meno, huku asilimia 62.8 wakiwa na magonjwa ya fizi, hali inayohitaji kuendelea kuwekeza katika kinga na huduma za afya ya kinywa.
Aidha, amewataka Watanzania kuchukua hatua za kutunza afya ya kinywa kwa kufanya uchunguzi wa meno mara kwa mara, kuzingatia usafi wa kinywa, lishe bora na kutafuta matibabu mapema.
Amesema uwekezaji katika huduma za kisasa za meno una nafasi muhimu katika kuongeza uwezo wa nchi kutoa huduma bora, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau wengine katika kuimarisha huduma za afya.