DKT. SAMIZI: TEKNOLOJIA IIMARISHE MIFUMO YA AFYA KWA WANANCHI
Posted on: October 1st, 2026Na Shaban Juma, WAF – Kigali, Rwanda
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence George Samizi, amesema matumizi ya teknolojia katika sekta ya afya yanapaswa kulenga kuimarisha mifumo ya afya ya msingi, kuongeza upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi na kujenga mifumo imara inayoweza kukabiliana na changamoto za kiafya barani Afrika.
Dkt. Samizi ameyasema hayo leo Oktoba 1, 2026 jijini Kigali, Rwanda, wakati akimwakilisha Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, katika Mkutano wa Afrika wa Teknolojia za Afya 2026, akisisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kujenga mifumo ya afya inayoongozwa na nchi, inayounganishwa, inayostahimili changamoto na inayomweka mwananchi katikati.
Amesema Tanzania inaona mjadala huo kuwa muhimu, ikizingatiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekabidhiwa jukumu la kuwa Kinara wa Umoja wa Afrika katika Afya ya Mama na Mtoto, huku Tanzania ikiendelea kushirikiana na Africa CDC, Tume ya Umoja wa Afrika, nchi wanachama na wadau katika kuimarisha ajenda ya afya ya mama, mtoto mchanga na watoto.
Dkt. Samizi amesema nguvu ya mfumo wa afya inapaswa kupimwa kwa namna unavyoweza kumhudumia mwananchi pale anapohitaji huduma, ikiwemo mama mjamzito kupata huduma bora kwa wakati, mhudumu wa afya ngazi ya jamii kutambua hatari na kumwelekeza mgonjwa katika ngazi stahiki.
Amesema matumizi ya mifumo ya kidijitali yanaweza kuwezesha taarifa za mgonjwa kufikishwa katika kituo kinachopokea rufaa bila kuanza upya, majibu ya maabara kuwafikia wahudumu wa afya kwa wakati na taarifa za matukio yasiyo ya kawaida ya kiafya kufikishwa kwa wahusika kwa haraka.
Amesema mabadiliko ya kidijitali hayapaswi kuangaliwa kama suala la teknolojia pekee, bali kama njia ya kufanya mifumo ya afya ifanye kazi kwa ufanisi zaidi, huku ikiambatana na uwekezaji katika miundombinu, mawasiliano, mifumo inayoweza kuingiliana, viwango vya pamoja, usimamizi salama wa taarifa za afya na kuwawezesha watumishi wa afya.