Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAZIRI MKUU AKABIDHI HUNDI YA TZS. 50MIL KWA MUHIMBILI ZILIZOTOKANA NA NBC MARATHON

Posted on: July 28th, 2024



Hospitali ya Taifa Muhimbili leo imepokea hundi ya TZS. 50 Mil kutokana na mbio za NBC Marathon 2024 kwa ajili ya kusaidia kujenga vyumba vya upasuaji kwa kina mama wajawazito hospitalini hapo.


Akikabidhi hundi hiyo Jijini Dodoma, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amewapongeza NBC kwa ubunifu wao uliowezesha kukusanya fedha na kuwekeza katika Sekta ya Afya kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha huduma hizo hapa nchini.


"Michezo au kufanya mazoezi kuna faida kubwa sana, leo hii tunaona Watanzania wanadhamini na kutambua kushiriki katika michezo mbalimbali, tuko na wataalam wa afya watasema umuhimu na faida ya kufanya mazoezi” ameeleza Mhe. Majaliwa


Ameitaka Wizara ya Afya kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wanaoandaa michezo ambayo inawaleta pamoja wananchi kwa lengo la kufikisha elimu na kusisitiza umuhimu wa jamii kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi.


“Takwimu kutoka Wizara ya Afya zinaonesha kuwa watu wenye magonjwa yasioambukiza wameongezeka ikiwemo kisukari, figo na afya ya akili na kuongeza kuwa tabia bwete ni kichocheo cha magonjwa yasioambukiza hivyo kwenye eneo hili ni muhimu kuzingatia ushauri wa wataalam ”, amesema Mhe. Kassim


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Prof. Mohamed Janabi amewashukuru NBC kwa kuandaa mbio hizo ambazo ni muhimu kwa afya lakini pia mchango walioutoa utasaidia kuendelea kuboresha maeneo ya kutolea huduma katika Hospitalini hapo.


“Kawaida kila mmoja wetu anatakiwa kutembea hatua elfu kumi kila siku kwani itakukinga na maradhi ya moyo, kisukari na itakuongezea afya ya akili kwa sababu afya ya mwili inategemea afya ya akili”, amesema Prof. Janabi.