Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MIUNDOMBINU BORA YA VITUO VYA AFYA YAONGEZA UBORA WA HUDUMA ZA UZAZI KIGOMA

Posted on: February 18th, 2026

Na Cletus Sanga, WAF – Kigoma


Uboreshaji wa miundombinu, ujenzi, ukarabati wa vituo vya afya na zahanati, pamoja na upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa na dawa, umeimarisha ubora wa huduma za uzazi, mama, na mtoto.


Hayo yamebainishwa leo, Februari 18, 2026, na Mkuu wa wilaya ya Kigoma mjini, mkuu wa mkoa, Dkt. Rashidi Chuachua, kaimu Mkuu wa mkoa wakati wa utambulisho wa Mradi wa mama mjamzito na Mtoto Salama mkoani Kigoma, unaotekelezwa na Shirika la Thamini Uhai kwa kushirikiana na Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI.


“Kupitia juhudi za pamoja, kiwango cha vifo vya akina mama kimepungua kutoka vifo 565 hadi kufikia vifo 104 kwa kila vizazi hai 100,000. Hali hiyo inaonesha mafanikio ya uwekezaji unaofanywa katika sekta ya afya,” amesema Mhe. Chuachua.


Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Bi. Monica Julius, amesema Serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha huduma za mama na mtoto zinaimarika. 


Bi. Monica amebainisha kuwa watumishi wa huduma za afya wamejengewa uwezo ili kuongeza ufanisi na ubora wa huduma zinazotolewa. 


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Thamini Uhai, Banzi Msumi, ameishukuru Serikali kwa juhudi kubwa zinazofanyika ili kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto nchini.


Ameeleza kuwa tangu mwaka 2016, Thamini Uhai ilitekeleza mradi wa msindikizaji wa mjamzito katika vituo tisa kama mradi wa majaribio katika halmashauri tano za mkoa wa Kigoma. Utekelezaji wa mradi umeendelea kusambaa, kwa sasa unatekelezwa katika vituo vya kutolea huduma kumi na sita (16) katika halmashauri zote nane za mkoa wa Kigoma kupitia ufadhili wa Foundation H&B Agerup, iliwemo vituo saba (7)vilivyoboreshwa kupitia mapato ya ndani ya mkoa. Mpango huo umechangia kuongeza mahudhurio ya wajawazito katika vituo vya afya.

Ameongeza kuwa mradi huu umeboresha miundombinu ya afya ya wodi za wazazi kuhakikisha usiri na heshima kwa wakina mama wakati wa kujifungua. Hatua hiyo imeongeza imani ya wajawazito kutumia huduma za uzazi katika vituo vya afya.


Aidha, Mradi huu mpya unaotambulishwa leo utaenda kuimarisha upatikanaji wa huduma jumuishi za dharura za afya ya mama na mtoto mchanga ikiwemo tiba kinga ya kuvuja damu wakati wa kujifungua, upanuzi wa huduma bora na matibabu ya Watoto wachanga, na huduma bora za kliniki ya wajawazito katika mkoa wa kigoma. Huduma hizo ni muhimu katika kukabiliana na changamoto za uzazi hatarishi.